Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema mtoto atakaye chelewa kuanza Masomo kwa wakati atalima matuta kumi.
hayo yamesemwa jana tarehe 04 Januari 2024 wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua Miradi ya ujenzi wa shule ya Sekondari ya Michese na kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Kata ya Mkonze eneo la Michese.
“Wazazi msiwasababishie watoto adhabu ya kulima matuta kumi kwasababu ya kuchelewa kufika shule kwa wakati na kuchelewa kuanza masomo wanafunzi wanaanza kusoma tangu siku ya kwanza wanapofungua shule”
“Dodoma tunataka ufaulu wa kiwango cha juu kama ilivyo hadhi ya Makao Makuu ya nchi yetu tunaendelea kufanya vizuri kwenye masomo na hatutaki kurudi nyuma” Amesema Senyamule.
Pia Mhe. Senyamule amekagua ujenzi wa shule ya Sekondari ya Michese unaotekelezwa katika kata ya Mkonze eneo la Michese na kuagiza kukamilika kwa ujenzi huo ili ifikapo tarehe 08 Januari wanafunzi waweze kukaa kwenye madarasa yenye ubora.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Justin Machela amesema tuwapeleke watoto wetu shule na kuepuka Malalamiko yasiyo na Msingi ili kuhakikisha watoto wanaanza masomo kwa wakati na kuwanunulia vifaa vinavyoitajika Shuleni kama madaftari na kalamu.
Vile vile Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkonze Bw. Andrew Rumishaeli amesema shule ya Sekondari Mkonze ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 544 ikiwa ni fedha za Sequip kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 08 vya madarasa vyenye ofisi 02, Jengo la Utawala, Jengo la maktaba, Jengo la Tehama, vyoo vya wanafunzi matundu 08, Kichomea taka na Tanki la maji la ardhini.