Theophilida Felician Kagera.
Wananchi wa Kata za Kanyigo na Kashenye wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera, wamehimizwa kutunza urithi wa kihistoria, utamaduni na malikale, na kuhakikisha urithi huo haupotei badala yake urithishwe kizazi hadi kizazi, kufahamu chimbuko lao.
Hayo yamesemwa na Dk Daniel K. Ndagala ambaye ni mdau wa Utamaduni na maendeleo nchini Tanzania, ambaye pia ni mmiliki na Mkurugenzi wa Nyumba ya Makumbusho Kanyigo(Kanyigo Museum), inayohifadhi malikale na kumbukumbu nyinginezo, wakati akiongoza matembezi ya kiutalii katika Kata za Kanyigo na Kashenye tarehe 30 Disemba 2023, kuvitembelea vivutio vya utalii na kuvitangaza kwa lengo la kuvitangaza ili viweze kutembelewa na watu wengi zaidi wakiwamo watalii kutoka nje.
Washiriki zaidi ya mia moja wakiwamo wanafunzi na watu wazima baadhi wakifuatana na watoto wao, wametembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria yakiwemo mapango yenye michoro ya kale, ufuaji chuma wa kale, Ukumbi mkubwa na wa
kisasa kwa ajili ya mikutano na shughuli mbalimbali utakaokamilishwa na upandaji wa maua anuai, maarufu kama Julieth Botanical Garden, mandhari za Ziwa Victoria nk.
Amewashauri walimu kuwaongoza wanafunzi wao kuyatembelea maeneo ya kihistoria kujifunza mambo mbalimbali, huku wakizingatia utunzaji wake, kadhalika viongozi wa vijiji kusimamia sheria ndogo ndogo za utunzaji mazingira kuhifadhi vivutio hivyo.
Matembezi yalihusisha watu tofauti na kila mmoja aliweza kutoa mchango wake, wenyeji walitoa historia ya maeneo husika na huku wataalamu wakitoa maelezo ya kitaalamu kuhusu nyanja za uchumi na maendeleo, akiwemo Prof. Benezeth Mutayoba aliyeshauri juu y a matumizi bora ya ardhi, huku wakili msomi Joseph Abel, ambaye ni mdau wa utalii, akieleza uzoefu wake kutokana na kutembelea maeneo ya utalii ya Serengeti, Ngorongoro, Manyara, Tarangire, Ruaha na Rubondo, na akashauri iwapo vivutio vya utalii alivyoviona kwenye ziara hii maarufu Chimbuko Kanyigo, iwapo vitazidi kutangazwa vitawaleta watalii wa ndani na nje kwani vina mandhari nzuri.
Julius Kassano, mmoja wa waliohamasisha matembezi hayo ya kiutalii yaliyomvuta pia ndugu Emmanuel Mwambe kutoka Mtwara Mikindani akiongoza timu ya watu 11 wakiwemo watoto saba, amesema lengo ni kuchochea maendeleo na mshikamano ,kukutana pamoja na kujadili fursa za kiuchumi.
Mgeni rasmi wa tukio hilo la utalii wa ndani, Kanali Ngemela Lubinga ambaye ni Mwenyekiti wa Shirika la maendeleo kata za Kanyigo na Kashenye, amewashukuru waandaaji wa matembezi hayo akisena ni njia mojawapo ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Tanzania, kupitia Royal Tour kuwaleta watalii wengi zaidi nchini, na mi matarajio yake kwamba vivutio hivi, vitaongeza idadi ya watalii.
Kanali Lubinga amewahimiza pia wananchi kujikita kwenye kilimo cha kahawa, kuzingagia misingi ya usafi tangu shambani, kuvuna na kuanika hadi uuzaji ili kuepuka kahawa ya wakulima kukataliwa na wanunuzi kwenye masoko kwa kutofikiwa viwango vinavyokubalika.