Home Kitaifa ATOA NYUMBA YAKE KUWA KITUO CHA POLICE

ATOA NYUMBA YAKE KUWA KITUO CHA POLICE

Na Neema Kandoro – Mwanza

Mfanyabiashara na mkazi wa kata ya Ilangala, kisiwa cha Gana, Wilaya ya Ukerewe amejitolea nyumba yake aliyokuwa anaitumia na kuikabidhi kwa Jeshi la Polisi ili iwe Kituo cha Polisi kwa ajili ya kutoa huduma za Usalama kwa wakazi zaidi ya 6,000 wa kisiwa hicho.

Nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya 15 inatakiwa kufanyiwa ukarabati mdogo wa kuwekewa miundombinu na mifumo ya majitaka itakayokidhi hadhi ya Kituo cha Polisi.

Akizungumza na Wananchi wa kisiwa hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Polisi katika eneo hilo kunaenda kutatua changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikiwakabili kisiwani hapo huku akimuomba mfanyabiashara huyo aliyejitolea kujenga kituo cha Polisi kukamilisha mapema hadi ifikapo mwishoni mwa Januari 2024.

Niwapongeze wananchi wa eneo hili kwa kukubali kujenga kituo cha polisi katika eneo hilo, ikiwezekana kabla ya mwishoni mwa mwezi Januari 2024 pengine kituo hicho kiwe kimekamilika na mimi nitatamani sana kuja kukizindua hiki kituo ili tuweke askari wa kutosha kuanza kufanya kazi,” amesema Kamanda Mutafungwa.

Hata hivyo, wakazi wa Kisiwa hicho wamemweleza Kamanda Mutafungwa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo na kuomba Serikali iwatatulie ikiwa ni kukithiri kwa vitendo vya mmonyoko wa maadili, ulevi, utovu wa nidhamu, wizi wa nyavu na injini za mitumbwi, uvuvi haramu, ukatili wa kijinsia, udokozi, mauaji, unyanyasaji na ukosefu wa alama za mipaka ziwani zinazoonyesha mpaka wa Tanzania na Uganda.

Aidha, wananchi hao wameliomba Jeshi la Polisi kusaidia kukamilisha mapema ujenzi wa kituo hicho ili changamoto hizo zitatuliwe huku wakiomba mipaka inayotenganisha Tanzania na Uganda iwekwe ziwani ili kupunguza matukio ya wavuvi wa pande hizo mbili kuingiliana.

Swai Somba, Mvuvi kisiwani hapo amemwomba Kamanda Mutafungwa kuharakisha ujenzi wa kituo hicho cha Polisi kutokana na changamoto ambazo wananchi wa eneo hilo zaidi ya 6,000 wamekuwa wakikumbana nazo.

Sisi wavuvi wadogo tunapotoka hapa Kisiwani kuingia Ziwani huko kuvua huwa tunanyanyasika sana kutokana na vyombo vyetu mfano sisi wavuvi wa kasia huwa uvuvi wetu ni duni lakini wanaotumia mashine wametuwekea masharti ambayo mimi ninashindwa kujua moja wapo ukitoka ziwani ukileta hapa samaki unaanza kuulizwa umetumia zana gani kuvua wakati huenda ulikuwa na ndoano, tunaomba msaada katika hili“, amesema Somba.

Kamanda Mutafungwa tunashukuru sana kwa ujio wako hapa Kisiwani na umesema unajua changamoto zinazotukabili, mimi ninataka nijue sisi wavuvi tunaoenda masafa marefu huwa tunasumbuliwa sana na wavuvi na askari wa Uganda wanaokuja huku kwetu kuvua na wakati mwingine wanatukamata na kutunyang’anya samaki na nyavu zetu je mipaka huko ziwani mnatuwekea lini ?,” aliuliza Kemelo Matiku, mvuvi katika kisiwa cha Gana.

Akijibu swali hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri na Uvuvi endelevu ziwa Victoria, Bakari Kadabi amesema, kuanzia Januari 2024 Serikali inatarajia kuweka mipaka ziwani itakayokuwa inawasaidia wavuvi kujua upande wa Tanzania na Uganda.

Kuhusu mipaka Serikali imejipanga kuanzia mwezi Januari kuweka maboya mpakani kati ya Tanzania na nchi jirani kwa hiyo tatizo la kuingilia linaenda kuisha kabisa ila niwaombe wavuvi muwe wakweli hamna sababu ya kwenda kuvua upande wa Uganda wakati huku tuna maeneo mengi ya kuvua,” amesisitiza Kadabi.

Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa ametangaza kufanya oparesheni kabambe na endelevu ndani ya Ziwa Viktoria na maeneo mengine ili kutokomeza uhalifu na kuimarisha ulinzi na usalama zaidi katika maeneo yote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!