Home Kitaifa Mhe. Kikwete awataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kushiriki...

Mhe. Kikwete awataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kushiriki kikamilifu mafunzo ya PEPMIS na PIPMIS

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb,) amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuzingatia mafunzo wanayopewa ili kuboresha utendaji kazi wa watumishi na taasisi kwa ujumla.

Mhe. Kikwete ameyasema hayo leo tarehe 19 Desemba, 2023 jijini Dodoma alipofungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kupima utendaji kazi wa mtumishi na taasisi ya PEPMIS na PIPMIS.

Mhe. Kikwete ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi ndio maana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imebuni mfumo huo unaolenga kutatua changamoto za upimaji utendaji wa watumishi, kujua mwelekeo wa taasisi kiutendaji katika kuwahudumia wananchi.

Nawapongeza sana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) pamoja na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na hasa kupitia kazi ya ukusanyaji maoni kwa ajili ya uandaaji wa Dira ya taifa ya mwaka 2050 ambayo itaenda kuonesha mwelekeo wa nchi kwa miaka 25 ijayo” Amesema Mhe. Kikwete.

Aidha, Mhe. Kikwete amesema kuwa mfumo wa upimaji uliokuwa ukitumika awali wa ujazaji wa fomu za OPRAS ambao ulianza mwaka 2004 ulionekana kushindwa kupima uhalisia wa kiutendaji, hivyo mfumo huu PEPMIS unapima utendaji wa watumishi sehemu ya PIPMIS unapima utendaji wa taasisi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Dkt. Tausi Kida amesema kuwa majukumu ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ni pamoja na kusimamia Tume ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina yenye mashirika zaidi ya 300, kusimamia sekta binafsi katika masuala ya sera na sheria katika uwekezaji kupitia Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji (EPZA).

Tunaishukuru sana Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kwa kuja na mfumo huu kwani utasimamia ufanisi wa kiutendaji na kuleta haki kwa watumishi wa umma, sisi tumeufurahia mfumo huu ambao utaenda kuongeza tija katika kuwahudumia wananchi na kuboresha maeneo ambayo yatakuwa na changamoto na kuongeza ufanisi” Amesema Dkt. Kida.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!