Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amewahakikishia wakazi wa Kata ya Mburahati ambao makazi yao yamekuwa yakikumbwa na mafuriko kuwa Serikali inaendelea kutatua changamoto hiyo kwa awamu.
Akiwa ziarani katika Kata ya Mburahati Dar es Salaam Mbunge huyo amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto ya mafuriko kwa baadhi ya Wananchi na ndiyo maana imekuja na mpango wa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kushughulikia changamoto ya mafuriko.
Prof. Kitila amesema hatua za muda mfupi ambazo zimekuwa zikichukuliwa ni kuondoa taka na mchanga kwenye mito inayosababisha mafuriko, huku hatua za muda wa kati zikiwa nikujenga kingo za mto kwenye maeneo hatarishi zaidi na hatua za muda mrefu ambazo zitachukua muda mrefu kutekelezwa ni kujenga kingo kwa mito inayosababisha mafuriko kwa mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli hiyo ya Prof. Mkumbo aliitoa kufuatia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Barafu Suphian Hamis Juma ambaye alieleza kuwa mpaka sasa nyumba 63 kwenye mtaa wake wananchi wamehama kutokana na mafuriko.
Amesema kufuatia kuhama kwa wananchi hao ambao walikuwa na mchango wa kiuchumi katika maeneo hayo pamoja na shughuli za kijamii kumesababisha kuzirota kwa shughuli za kiuchumi.
Baadhi ya Wananchi waliochangia hoja hiyo akiwemo Mwanaasha Haji na Shaban Tinda ambaye ni Mjumbe wa Shina namba 4 Mtaa wa Barafu wamesema pindi mawingu yanapotanda wamekuwa wakigubikwa na hofu.
Wamesema ujio wa Mbunge wao Prof. Kitila Mkumbo umewapa faraja maana mara zote anapotoa ahadi zake amekuwa akizitekeleza hivyo wanaamini ahadi yake itatatua changamoto zao.
Katika ziara hiyo Mbunge Prof. Kitila Mkumbo kwa kushirikiana na Diwani wa Kata ya Mburahati Omari Yusuph Yenga wameahidi kupeleka gari la kutoa mchanga kwenye daraja la Pipo Mburahati.