Ashrack Miraji Same kilimanjaro
Katika kuadhimisha Siku ya kumbukizi ya Miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania bara Mkuu wa wilaya ya Same Kasilda Mgeni ameshiriki na viongozi wengine pamoja na baadhi ya wananchi wakazi wa wilaya hiyo katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kufanya usafi na upandaji Miti zaidi 300 kwenye maeneo tofauti yenye vyanzo vya maji hikiwemo Hospitali ya Wilaya hiyo ya Same
Mkuu huyo wa wilaya amewataka wakazi wa wilaya hiyo pamoja na jamii kwa ujumla kuendeleza umoja na mshikamano, kudumisha tunu ya taifa iliyo dumu kwa miaka yote zaidi ya 62 tangu Nchi ya Tanzania kupata uhuru wake suala ambalo limekua likitolewa msisitizo na viongozi mbalimbali.
‘Niwaombe viongozi wenzangu na wananchi kwa ujumla wetu tushirikiane hasa suala la kutunza mazingira na usafi kwa ujumla wake, tulisha jiwekea utaratibu wa kila kaya kupanda miti kwenye maeneo yetu lakini tunafahamu yapo maeneo ya wazi na taasisi mbalimbali za Umma suala hili litasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi hasa ukame na Mmomonyoko wa ardhi kwenye wilaya yetu” Alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Amewataka pia wakazi wa wilaya hiyo kutambua kuwa maadhimisho ya Uhuru yanalenga kukumbusha wajibu wa kila mtanzania ikiwemo umuhimu wa kulinda Rasilimali za nchi na uzalendo kwa taifa , suala ambalo ndio msingi wa kuyafikia maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwaombea viongozi wakuu wa Nchi hasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
“Niwaombe wananchi wenzangu tuendelee kuunga mkono serikali yetu inayo ongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan, kuadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania pamoja na mchakato wa ukusanyaji maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa kuelekea mwaka 2050” Alisisitiza