Waziri wa Nchi OR-MU Prof. Kitila Mkumbo baada ya kutembelea Kata ya Manzese hapo jana, hii leo amekwenda Kata ya Makuburi ambako ametembelea kituo cha afya cha Makuburi na kuona namna huduma zinavyoendelea kutolewa.
Akiwa katika kituo hicho cha afya kipya ambacho ni miongoni mwa ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2020 juu ya kuboresha huduma za afya, amesema kituo cha afya Makuburi kitaendelea kuboreshwa zaidi.
Prof. Kitila Mkumbo amesema pindi huduma za mama na mtoto zitakapoanza kutolewa, Serikali itaongeza idadi ya wakunga na wauguzi ili kuwezesha huduma kutolewa bila vikwazo kwa wananchi.
Mganga Mkuu katika kituo hacho Elizabeth Kalinga amesema kwa sasa kituo hicho cha afya kinatoa huduma kwa wagonjwa wa nje pekee kutokana na kutokamilika na kumuomba Mbunge kuwasaidia kupatiwa vifaa tiba na vitendanishi ombi ambalo Prof. Kitila ameridhia kulifanyia kazi.
Kuhusu ujenzi wa Zahanati ya Makoka, amesema kwa kuwa tayari eneo limeshatolewa na Jeshi, taratibu za ujenzi zitaanza ili wananchi wasipate shida ya kufuata mbali huduma za afya.
= = = = = =