Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari ya mapema kupitia mifumo, Sera na Teknolojia. Amesema hayo wakati akizungumza kwenye Jukwaa la Mawaziri la Majadiliano ya Juu la Utekelezaji wa Tahadhari ya Mapema kwa Wote katika Mpango Kazi wa Afrika lililofanyika pembeni ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Dkt. Jafo amesema Serikali inahakisha inapunguza athari za majanga kwa kuboresha ustawi na uthabiti wa watu wake na jamii kama sehemu ya mkakati wa maendeleo kwani majanga matokeo ya maafa yanaathiri mipango na malengo ya maendeleo yake.
“Ni muhimu kujiandaa kupitia mifumo ya tahadhari ya mapema inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa athari na kuokoa maisha ya watu na mali nyingi na kwa umuhimu huo Tanzania imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021-2026) pamoja na Mchango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi (NDC),” amesema.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa Serikali ya Tanzania ilitunga Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya mwaka 2019, inayotoa maelekezo na kuimarisha mamlaka ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoa Huduma za Tahadhari za Mapema.
Ameongeza kuwa Serikali pia ilikuja na Mifumo ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (NFCS), ambayo ilizinduliwa Agosti 2018 sanjari na kufunga rada saba za hali ya hewa na tatu za hali ya Hewa tayari zimeanza kufanya kazi.
Hata hivyo, Dkt. Jafo amesema imeanzishwa shahada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu masuala ya Hali ya Hewa na Mabadiliko ya Tabianchi, kusaidia kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu nchini hasa kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Kutokana na taarifa za hali ya hewa kutoka TMA, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara na Wadau wote wenye dhamana iliandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa El Nino na hatua ya matarajio Agosti, 2023 ambao umechangia kupunguza athari za mvua hizo.
“Nachukua fursa hii kuthibitisha dhamira ya Tanzania ya kufanya kazi na WMO, wadau, na Wanachama wengine wa WMO katika kuboresha uwezo wa Mamlaka zetu za Hali ya Hewa kwa manufaa ya watu wetu na mataifa yetu,” amesema Dkt. Jafo huku akibainisha kuwa TMA inatoa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa hadi zaidi ya asilimia 86. Hivyo amesema, TMA inaboresha uwezo wa kufanya kazi kwa watumishi wake ambapo asilimia 14.5 wamepewa ujuzi na maarifa juu ya programu za hadhari katika taasisi mbalimbali za mafunzo ndani na nje ya Tanzania.