Kushirikiana na Makampuni bingwa ya Ushauri nchini kuitangaza sekta ya madini
Wizara ya Madini kufungua Dawati maalum la Uwekezaji TIC
Kufungua kiwanda cha uchenjuaji kitakacho hudumia Ukanda wa Sub Sahara Afrika
Wizara ya Madini imepanga kuweka mikakati shirikishi ya uwekezaji katika Sekta ya madini itakayowavutia na kuwanufaisha wachimbaji wadogo,wa kati na wakubwa.
Hayo yamebainishwa Novemba 21, 2023 na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali wakati akizungumza na uongozi wa kampuni ya BHP na Lifezone katika mkutano wa biashara baina ya Tanzania na Uingereza unaoendelea jijini London.
Sambamba na hapo, amesema wizara ya madini itaandaa mpango wa mafunzo maalum yaani Apprenticeship Program katika maeneo kazi kwa maafisa ili kuongeza ujuzi na maarifa kwenye mnyororo mzima wa uwekezaji ndani na nje ya nchi.
Mahimbali ameongeza kuwa , wizara ya madini kwa kushirikiana na kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itafungua Dawati maalum la uwekezaji kwa ajili ya kuratibu shuguli za uwekezaji ndani ya sekta ya madini.
Akielezea kuhusu ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji madini mkakati, Mahimbali ameeleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya BHP Group Limited na Lifezone Metals kupitia kampuni tanzu ya Tembo Nickeli imepanga kujenga kiwanda kikubwa nchini Tanzania cha uchenjuaji madini mkakati yatakayochimbwa katika nchi zilizo Ukanda wa Sub Sahara Afrika.
Akiwa ameambatana na wataalam kutoka wizara ya madini, Mahimbali amesema kuwa Wizara ya Madini imeridhishwa na mwamko ulioneshwa na wawekezaji wa nchini Uingereza na kuahidi kutoa kushirikiana mzuri kwa faida ya nchi zetu.
Akizungumzia maendeleo na ukuaji wa sekta ya madini nchini , Mahimbali amebainisha kuwa kwa mwaka 2022 Sekta ya Madini imekuwa kwa asilimia 10.9 na imechangia asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa na kuingiza asilimia 56 ya fedha zote za kigeni nchini.
Aidha, akielezea kuhusu mafanikio ya ziara hiyo, Mahimbali amesema kuwa timu ya wataalam imejifunza mambo mbalimbali ya kibiashara ikiwemo umuhimu wa wachimbaji madini kuwa na taarifa nzuri za biashara zinazoweza kushawishi uwekezaji , kuongeza uratibu wa takwimu za kitaifa zinazohusu sekta ya madini na kuwajengea ujuzi na maarifa maafisa ili waweze kuhudumia wawekezaji kwa kiwango kinachotarajiwa kimataifa.
Vilevile, Mahimbali amewashukuru watanzania wanaoishi nchini Uingereza (Diaspora) kwa ushirikiano wao waliouonesha katika kufanikisha ziara hii na kuaahidi kuwa wizara itateua Afisa Dawati Maalum la Madini ambaye atakuwa ndani ya Kituo cha Uwekezaji kwajili ya kushughulikia uwekezaji sekta ya madini.
VISION 2030: MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI