Na Scolastica Msewa, Kibaha
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amewataka Wazazi wa wazawa wa Mkoa wa Pwani kusomesha watoto wao ili waweze kunufaika na fursa za uwekezaji mkubwa unaoendelea Mkoani Pwani.
Akihutubia Wananchi wa mkoa wa Pwani wakati Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani ilipofika kukagua utekelezaji wa Ilani katika Shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Mkuza iliyopewa jina la Msimbo huko maeneo ya Msangani Kibaha mkoani Pwani amesema Serikali tayari imetimiza wajibu wake wa kujenga Miundo Mbinu ya elimu kilichobaki ni Wazazi kuwapeleka shule na kuwasimamia watoto wa wapate elimu.
Ameendelea kusema kuwa kazi kuu ya mtoto ni kumsomesha na si kumfisadi kwa kumpatia kazi ambazo zitamwingiza kwenye vitendo vitakavyomkatiza masomo yake.
Mlao alitaja baadhi ya shughuli ambazo Wazazi wa mkoa wa Pwani huwafisadi watoto wao kuwa ni pamoja na uuzaji wa biashara za mikononi Barabarani, upigaji debe wa mabasi ya abiria barabarani badala ya kwenda shule kupata elimu.
Aidha Mlao alimpongeza Mhe. Daktari Samia Suluhu Hassan Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuonyesha Uzalendo wa kulithamini Taifa lake kwa kutoa fedha nyingi zinazotekeleza miradi ya maendeleo.
Awali wakiwa Katika Bandari Kavu ya Kwala Meneja msaidizi wa mradi wa Bandari Kavu Kwala Eng. Gabriel Mwangosi amesema lengo la kuanzishwa kwa bandari hiyo ni kupunguza asilimia 30 ya msongamano wa makontena katika Bandari ya Dar -es – Salaam na kutengeneza Mazingira mazuri ya huduma za Bandari kwa wateja wao hususani mataifa mbalimbali yanayohudumiwa na Bandari ya Dar -es – Salaam.
“Kinachotakiwa Bandari iwe inapumua kwa makontena mengine kuondolewa na kuruhusu makontena mengine Kuingia, ambapo itasaidia uharaka wa kupakua makontena kwenye meli na unapotaka kupima ubora wa Bandari ni kushusha haraka na kupakia haraka ili dhamira ya Serikali na Chama itimie” alisema Mwangosi.
Ameendelea kusema kuwa yale mataifa yanayohudumiwa na Bandari ya DSM kama nchi yamepewa maeneo yao katika eneo hilo la Bandari Kavu ya Kwala ambazo ni nchi za Rwanda, Zambia, Congo lengo likiwa ni kushusha makontena 3000 kwa Siku sawa na Makontena laki 8 kwa mwezi.
Akizungumzia kuhusu mradi wa Kongani ya Viwanda Mwenyekiti wa SINO TAN ndg Jauson Huang amesema mradi huo ulianza mwezi may 2022 huku ukiwa na awamu tatu hadi kukamilika, ingawa awamu ya kwanza inatarajia kumalizika mwezi Desemba 2023.
Huang ameendelea kusema kuwa mradi huo utakapokamilika utatoa faida ya kuajiriwa kwa wafanyakazi laki 1.
Aidha Kamati hiyo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibaha ilikagua Maendeleo na huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Wilaya hiyo ili iweze kutoa huduma kwa ufanisi inahitaji kuwa na korido zinazounganisha jengo Moja kwenda jingine yenye urefu wa MITA 915 kufanya zaidi ya milioni 523 zinahitajika ili kukamilisha mpango huo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kibaha Dr. Christopher Ngendello amesema hadi kufikia October, 2023 jumla ya wagonjwa 5272 wamehudumiwa katika Hospitali hiyo.
Akizungumzia tangu kuanza kwa huduma ya X Ray na Ultra Sound Hospitalini hapo kumepunguza Idadi ya Rufaa zinazoenda Hospitali ya Mkoa ya Tumbi na kuweza kutibiwa Hospitalini hapo ambapo wagonjwa waliopatiwa huduma ni 759, kati Yao X ray ni 589 na Ultra sound 170.
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani ikiwa katika Halmashauri ya Mji Kibaha ilifanikiwa kutembelea na kukagua Utekelezaji wa Ilani Katika miradi ya Shule mpya ya Sekondari ya Shimbo Mkuza, Ujenzi wa barabara kwa kiwango Cha lami yenye urefu wa Km. 0.7 iliyopo picha ya ndege – Bokotimiza yenye thamani ya Shilingi bilioni 1 kupitia tozo za mafuta, na Soko la Kisasa lililopo katika Kata ya Tangini ambalo limekamilika kwa asilimia 99.5 na kugharimu jumla ya shilingi bilioni 8.