Na Shomari Binda-Musoma
KATIBU wa NEC, Uenezi, Itikadi na Mafunzo wa CCM Taifa Paul Makonda amesifu na kupongeza mchango wa Profesa Sospeter Muhongo.
Amesema elimu aliyokuwa nayo amekuwa akiitumia vizuri kwa kutoa ushauri kwa serikali katika masuala mbalimbali.
Makonda amesema viongozi mfano wa Profesa Muhongo wanahitajika nchini katika kuishauri serikali katika kuona taifa linasonga mbele.
Akizungumza kwenye kikao cha wazee ukumbi wa CCM mkoa amesema wazee lazima wasikilizwe na kupokea ushauri ili kutekeleza vyema majukumu.
“Nimefarijika sana kuonana na mzee wangu profesa Muhongo ambaye ushauri na mchango wao unahitajika ndani ya taifa letu”
“Wazee ni hazina katika taifa letu ambao tunapokea ushauri wao na lazima tutenge muda wa kuwasikiliza ili kupata ushauri wao” amesema Makonda.
Amesema maneno ya wazee kwa watoto yanamfikia Mungu na kuwapa nafasi ya kufanya kazi katika kuwatumikia wananchi.
Makonda amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa wazee na kuomba kuendelea kumuombea katika kuliongoza vyema taifa.
Amesema katika ziara yake ameona upo uzembe kwa watumishi serikalini ambao upelekea wananchi kuilalamikia serikali na Chama cha Mapinduzi.
Ameongeza kuwa Rushwa imekuwa kama utaratibu wa kawaida na kwenye chama kama hauna pesa huwezi kupata nafasi ya uongozi.