Na Neema Kandoro, Mwanza
WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa hati zaidi ya 300 kwa siku mbili katika Halmashauri ya jiji la Mwanza kupitia huduma ya Kliniki ya Ardhi.
Akizungumza leo Jijini Mwanza katika mwendelezo wa utoaji wa huduma hiyo Kamishina Msaidizi wa Ardhi Mkoani Mwanza Happiness Mtutwa alisema kuwa Lengo la huduma hizo ni kuhakikisha kuwa watu wote katika eneo hilo wanaondokana na changamoto ya Ardhi Ili waendelee na Shughuli za uzalishaji mali.
Mtutwa alisema kuwa wamepokea maelekezo ya Waziri Mwenye dhamana ya kuhakikisha kuwa changamoto za Ardhi zinapatiwa suluhisho la kudumu.
Mkuu wa wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi alisema matatizo ya ardhi yalikuwa yanamnyima usingizi na kumfanya kutumia siku mbili kwa juma kusikiliza kero zake.
Aliwataka watumishi wa idara hiyo kufanya kazi kwa juhudi ili kupatikane kwa suluhu ya matatizo yote ya ardhi ili kuruhusu wananchi kutumia muda wao katika uzalishaji mali.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji Jiji la Mwanza Catres Rwegasira alisema wameweka lengo la kutoa hati miliki zaidi ya 1000 na vibali 200 katika muda wa huduma ya kiliniki ya ardhi kwenye Halmashauri hiyo.