Na Shomari Binda
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo ameshauri mipango ya serikali ilenge kupunguza na kuondoa umasikini kwa kasi kubwa.
Ushauri huo ameutoa bungeni wakati akichangia mapendekezo ya mpango wa taifa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema ili kuondokana na umasikini kwa wananchi uchumi unapaswa kukua kwa kasi ya asilimia 8-10 (8-10%) ili kupunguza umaskini kwa kasi kubwa
Muhongo amesema Mipango na Bajeti vishughulikie mahitaji muhimu ya kila siku ya watanzania kama chakula, maji, umeme na matibabu katika zahanati,vituo vya afya na hospital.
Amesema vipimo vya upatikaji wa huduma muhimu kwa vile maji na umeme, viweke maanani matumizi halisi ya mtu mmoja mmoja kwa mwaka
“Mipango lazima iwe na sura mbili ili mafanikio yake yapatikane kwa harakan kuweza kuwaondoa wananchi wetu kwenye umasikini”
“Tujielekeze kwenye uchumi unaokua kwa zaidi ya asilimia 6 na duniani kote wameweza kufanikiwa kwa uchumi kukua kwa asilimia 8 hadi 10” amesema Muhongo.
Amesema kwa sasa takwimu zinaonyesha hapa nchini asilimia 18.7 ya wananchi wapo kwenye hali ya chini ya chakula kwa hiyo mipango na uwekezaji lazima ilenge kuondoa umasikini.
Muhongo ameshauri kuwa yapo maeneo ambayo yakielekezwa kwenye mpango zipo fedha za haraka za kupambana na umasikini ikiwa ni pamoja ns gesi,kilimo na uvuvi pamoja na madini yanayohitajika duniani.
Mbunge Muhongo amesema hayo yote yatawezekana iwapo kutakuwa na elimu bora kila ngazi lakini akaonyesha wasiwasi kwa halmashari kutekeleza mpango wa sera ya elimu iliyopangwa kutekelezwa kuanzia mwaka 2027.