Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Ali Mohammed Shein amefurahishwa na taarifa ya maendeleo ya Chuo hicho iliyowasilishwa kwake na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha leo Novemba 08, 2023.
Katika kuwasilisha taarifa hiyo uongozi wa Chuo umeongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Prof. Saida Yahya Othman na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha ambao wamemtembelea Mkuu huyo wa Chuo kwa lengo la kutoa taarifa ya Maendeleo ya Chuo kwa kipindi cha miezi sita yaani (mwezi Mei – Novemba, 2023)
Prof. Mwegoha amesema Chuo kinatarajia kuanzisha kituo cha mafunzo na mitaala kwa ajili ya Uongozi na Menejimenti (Centre for Leadership and Governance) kwa lengo kutoa mafunzo kwa viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, amemtaarifu Dkt. Shein kuhusu udahili wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika mwaka wa masomo 2023/2024 na kuanisha kuwa hadi kufikia mwezi Oktoba 2023 wanafunzi waliodahiliwa kwa kozi mbalimbali ni 7887.
Aidha, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William Mwegoha amesema katika mahafali ya 22 ya Chuo yanayotarajiwa kufanyika Mwezi Novemba na Desemba mwaka huu katika Kampasi za Morogoro, Mbeya na Dar es Salaam jumla ya wahitimu 3943 watatunukiwa Astashahada, Stashahada na Shahada mbalimbali.
“Nafurahi kukutaarifu kwamba kati ya wahitimu hao asilimia 51.46 ni wanawake na asilimia 48.54 ni wanaume” Mwegoha amefafanua.
Akizungumza na viongozi hao Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mkuu wa Chuo, Dkt. Ali Mohammed Shein amefurahishwa na mafanikio ya Chuo na kuwataka viongozi hao kuhakikisha wanatoa msukumo madhubuti katika ujenzi wa hosteli ya wasichana Ndaki ya Mbeya ikiwa ni agenda ya dhati ya kuweka mazingira bora ya kusoma kwa watoto wa kike.
“Ujenzi wa Hosteli ni muhimu sana kwa wanafunzi wa kike na takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu wa wanafunzi wa kike nchini unaongezeka. Hivyo juhudi za kuendeleza ujenzi wa hosteli ni juhudi zenye maslahi mapana kwa nchi yetu katika kuweka mazingira wezeshi ya kujifunzia” Amesisitiza Dkt. Shein.