Na Shomari Binda-Musoma
WAKULIMA kutoka mikoa ya kanda ya ziwa na nje ya mikoa hiyo wanatarajiwa kupewa mafunzo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 40 ya shughuli za kilimo za shirika hilo.
Mafunzo hayo yataendana na maonyesho ya shughuli za kilimo zinazofanywa na wakulima wanaotarajiwa kushiriki maonyesho hayo.
Maonyesho hayo ya shughuli za kilimo mseto yatafanyika kwenye kituo cha mafunzo ya kilimo mseto kilichopo Bweri manispaa ya Musoma kuanzia novemba 16 hadi 18.
Katika maonyesho hayo shirika la Vi-Agroforest litakuwa likiadhimisha miaka 40 ya shughuli zake katika kuwasaidia wakulima wa Tanzania.
Mmoja wa waratibu wa maonyesho hayo Davis Dominick amesema maandalizi yanaendelea vizuri ili kufanikisha maonyesho ya mwaka huu.
Amesema licha ya wakulima kushiriki maonyesho hayo watapata fursa ya kupewa mafunzo ili kulima kilimo chenye tija.
“Maonyesho ya mwaka huu yanaendana na maadhimisho ya miaka 40 ya shughuli za Vi-Agroforest kwa hiyo zipo shughuli ambazo zitafanyika”, amesema Davis.
Amesema katika ufunguzi wa maonyesho ya mwaka huu yanatarajiwa kufunguliwa na Katibu mkuu wa Mifugo na Uvuvi Profesa Riziki Shemdoe novemba 16 ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Pahali miti ustawi watu ustawi”.
Aidha mratibu huyo amewaomba wakulima na wananchi kujiandaa kushiriki maonyesho hayo ili waweze kujifunza masuala mbalimbali ya kilimo mseto.