Home Kitaifa PWANI WAZINDUA MNADA WA KOROSHO KWA KUUZA TANI 3854 KWA BEI YA...

PWANI WAZINDUA MNADA WA KOROSHO KWA KUUZA TANI 3854 KWA BEI YA SHILINGI 2094.46 KWA KILO

Na Scolastica Msewa, Kibiti.

Chama kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa mkoa wa Pwani CORECU kimezindua mnada wa korosho wa mwaka 2023/24 kwa kuuza tani 3854 kwa bei ya shilingi 2094.46 ambapo tani zaidi ya 20,000 za Korosho zinatarajiwa kuuzwa katika mkoa mzima wa Pwani.

Akitangaza bei ya korosho kwenye mnada huo wa uzinduzi uliofanyika wialayani kibiti mkoani Pwani Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika wa Wakulima mkoa wa Pwani CORECU Mantawela Hamisi amewataadharisha wakulima kukausha korosho zao ili zikauke vizuri waje kuuza kwenye ubora na bei nzuri sokoni hasa kwa kipindi hiki mvua za vuli zikiwazimeanza.

Amesema kama korosho za mkoa huo zingekaushwa vizuri hata katika mnada huo wa uzinduzi wangeuza bei kubwa zaidi ya walivyouza kwa bei ya shilingi 2094.46 kwa kilo.

Mnada huo uliohusisha wakulima na wadau mbali mbali wa zao la Korosho na wanunuzi ambapo Mkuu wa wilaya ya Kibiti Kanali Joseph Kolombo alikuwa mgeni rasmi akimwakirisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani mheshimiwa Abubakari Kunenge.

Kanali Kolombo amewataka wakulima kuzuia utoroshaji wa zao hilo kwenda kuuza katika mikoa jirani na kukosesha mkoa wa Pwani na halmashauri zake mapato.

Aidha kanali Kolombo amevitaka vyama vya msingi kuwasaidia wakulima wanaopeleka korosho zao kwenye maghala kuchambua na kuhakikisha wakulima wamekausha vizuri korosho zao.

“Yaani vyama vya msingi wasipokee korosho mbichi pale, mkulima yeye anachotaka ni kuuza korosho zake hivyo mwelekeze vizuri mkulima ajue namna ya kuziandaa vizuri ili auze korosho zae zikiwa zimekauka zikubalike sokoni na zinunulike vizuri” amesema Kanali Kolombo.

Hatahivyo Mkuu huyo wa wialaya ya Kibiti amewataka wanunuzi na Mabenki kuwalipa wakulima mapema kwa haraka ili wakulima wakaendelee na maandalizi yao ya kilimo cha mazao ya chakula kwa kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Aidha Kanali Kolombo amewataka wakulima wilaya ya kibiti kuhakikisha wanalima mazao ya chakula ya Mpunga, mahindi na mihogo angalau heka nne ikiwa ni pamoja na kuanza kulima zao jipya la biashara la mbaazi.

Amesema halmashauri ya kibiti imejipanga kugawa bure mbegu za mbaazi kwa wakulima na mwezi januari mwakani wanatarajia kufanya ukaguzi wa kuhakiki kama kila mkulima amelima mazao ya chakula mwaka huu.

Mwenyekiti wa Chama kikuu cha Ushirika wa Wakulima mkoa wa Pwani CORECU Musa Mngeresa amevitaka vyaka vya msingi vya wakulima mkoa huo kusimamia ubora wa korosho zinazopelekwa kwenye maghala yao kwa kulinda ubora wa korosho.

Meneja wa tawi la Dar es salaam wa bodi ya korosho Tanzania CBT Domina Mkangara wakulima wajitahidi kukabiliana na hali ya hewa ya mvua zilizoanza kunyesha ili kulinda ubora wa korosho zao kwa kuhakikisha wanaokota korosho zao kila siku.

“Wakulima tuhakikishe tunaokota korosho zetu kila siku yaani korosho inayoanguka inaokotwa siku hiyo hiyo isilale pale shambani bila kuokotwa kwasababu zikilala pale na hizi mvua zinazoendelea kunyesha tutapata changamoto kubwa ya unyevu utakaosababisha korosho kuoza hivyo tuzingatie kuokota siku hiyo hiyo” amesema Domina.

Naye mwakirishi wa Mrajisi wa vyama vya Ushirika mkoa Pwani Amas Chacha amewataka wakulima kuwasilisha korosho kwenye maghala ya vyama vya msingi mara mapema kwani kadri wanavyochelewa kupeleka korosho ghalani ndivyo maandalizi ya minada yanakuwa magumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!