Home Kitaifa Shirika la bima (NIC) laja na neema kwa Vikundi

Shirika la bima (NIC) laja na neema kwa Vikundi

SHIRIKA la Bima (NIC) limewataka watanzania walio katika vikundi kujiunga katika mfuko unaohudumia misiba ili waweze kumudu matukio hayo yanayojitokeza kwa ghafla na kuleta usumbufu kwa jamii.

Wito huo umetolewa leo Jijini Mwanza na Meneja NIC Kanda ya Ziwa Stella Marwa akitaja Bima hiyo iitwayo Group Funeral Cover kuwa inaweza kusaidia watu kuhudumia misiba inayojitokeza kwani watu wote wanaweza kumudu uchangiaji wake kwa kuwa ni mdogo.

Marwa alisema kuwa mwanachama anayejiunga na bima hiyo anaweza kuchagua dirisha atakalo ambapo mtu mmoja atachangiwa katika bronze sh 3000, silver 5000 na gold 8000 kwa kila mwezi.

Alisema mwanachama anayejiunga na bima hiyo anaweza kusaidiwa muda wowote panapojitokeza changamoto ya msiba ambapo hutolewa hadi kiwango cha sh milioni saba kugharamia mazishi.

Marwa alisema bima hiyo inawapatia wananchi unafuu kwani inapotokea msiba NIC hutoa fedha taslimu ambazo zinaweza kutumika kugharamia mazishi ya munufaika, wanafamilia ambao ni watoto wanne, mama na baba vilevile wazazi wote wa mwenza wa mnufaika.

“Bima hii ya serikali inahudumia hata mtu mmoja na Shirika hili la Umma limetimiza miaka 60 tangu kuundwa kwake hivyo tunawakaribisha watu wote kujiunga nasi” alisema Marwa.

Marwa aliwataka wananchi wote ndani ya Kanda ya Ziwa kujiunga na mfuko huo ili waweze kuondokana na msongo wa mawazo nyakati wanapokumbana na changamoto ya misiba kwenye familia zao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!