Na Shomari Binda-Musoma
WANANCHI wa Kisiwa cha Rukuba kilichopo kwenye jimbo la Musoma vijijini wameanza ujenzi wa shule ya sekondari ili wanafunzi waweze kusomea hapo.
Kwa sasa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wanalazimika kuvuka maji hadi nchi kavu Kata ya Etaro kuendelea na elimu ya sekondari.
Sekondari mpya tano (5) zinajengwa kwenye vijiji vitano ikiwemo Kisiwa cha Rukuba (Kata ya Etaro), Nyasaungu (Kata ya Ifulifu), Kurwaki (Kata ya Mugango), Muhoji (Kata ya Bugwema), na Wanyere (Kata ya Suguti huku serikali ikigharamia ujenzi na michango ya wadau na wananchi.
Wakizungumza kwenye eneo la ujenzi wakazi wa kisiwa hicho wamesema.sekondari hiyo inakuja kuwa mkombozi wa watoto wao.
Wamesema kuanza kwa ujenzi huo wanamdhukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa kuhamasisha ujenzi wa sekondari.
Hivi karibuni harambee ya kwanza ya ujenzi wa sekondari ya Kisiwa cha Rukuba ilifanyika chini ya usimamizi wa mbunge wa jimbo la Musoma Vijijini Profesa Sospeter Muhongo akishirikiana na Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya ya Musoma Vijijini.
Tayari mbunge Muhongo alishatoa mifuko 100 ya saruji na hii leo anatoa mifuko mingine 50 ili kuendeleza ujenzi huo kwa kasi.
Ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja ya walimu umeanza msingi wa mawe ukijengwa ili kuweka uimara wa majengo ya sekondari hiyo.
Wadau na wazaliwa wa kisiwa hicho wameendealea kuombwa michango kupitia akaunti kwenye Benji ya NMB kwa namba 30302300701 jina la akaunti serikali ya Kijiji cha Rukuba.
Wakazi wa Kisiwa cha Rukuba wamedhamiria kujenga sekondari kisiwani humo ili kuboresha upatinakaji wa elimu ya sekondari kwa watoto wao na kuomba kuungwa mkono.