Home Kitaifa WANANCHI VIJIJI VYA MAYANI, TEGERUKA NA KATARYO WAMSHUKURU PROF. MUHONGO KWA MRADI...

WANANCHI VIJIJI VYA MAYANI, TEGERUKA NA KATARYO WAMSHUKURU PROF. MUHONGO KWA MRADI WA MAJI

Na Shomari Binda-Musoma

WANANCHI wa vijiji 3 vya Mayani,Tegeruka na Kataryo wamemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo kwa juhudi za ufatiliaji kufikishiwa huduma ya maji.

Licha ya kumshukuru mbunge huyo wamewashukuru pia viongozi wa wilaya ya Musoma wakiongozwa na mkuu wa Wilaya Dk.Halfan Haule kwa kufatilia miradi ikiwemo ya maji.

Kauli hiyo wameitoa kwenye Kijiji cha Mayani wakati Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Musoma ilipotembelea na kukagua mradi wa maji unaoendelea kutekelezwa.

Katika mradi huo zaidi ya wakazi 13,200 wa vijiji vya Mayani,  Tegeruka na Kataryo wanatarajiwa kuondokana na adha ya kutembea zaidi ya saa sita kwenda ziwani na kurudi kufuata maji baada ya kukamilika kwa mradi wa usambazji wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi 4.699 bilioni.

Mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji Ssafi na Usafi wa Mazingira Musoma(MUWASA) unatarajiwa kukamilika mwezi novemba mwaka huu na unatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 13,200.

Akitoa taarifa kwa kamati ya Usalama ya wilaya ya Musoma iliyofanya  ziara kukagua maendeleo ya mradi huo Mkurugenzi wa Muwasa, Nicas Mugisha amesema hadi sasa mradi huo umefikisha asilimia 57.1 za utekelezaji wake..

Hata hivyo amesema mradi huo unakabiliwa  na changamoto kadhaa ikiwemo kuchelewa kwa malipo ya mkandarasi licha kuomba fedha za malipo ya kazi ambazo zimekwishafanyika.

“Tumeambiwa kwasasa pesa zipo tayari hivyo malipo yanatarajiwa kufanyika muda wowote lakini ifahamike mkandarasi huyu tangu ameanza kazi hajalipwa kiasi chichote na hadi sasa anadai zaidi ya Sh1.3 bilioni alizoomba tangu Juni,” amesema.

Wakizungumzia katika kijiji cha Mayani kuhusu upatikanaji wa maji kijijini kwao, baadhi ya wakazi wa kijiji  hicho  wamesema wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu hivyo mradi huo ni mkombozi kwao

Agnes Majura, amesema ukosefu wa maji katika kijiji chao ni changamoto  iliyodumu kwa muda mrefu hivyo kushukuru serikali kwa uamuzi wa kutekeleza mradi huo.

“Hebu fikiria unatumia muda wote huo wa saa sita kufuata ndoo moja tu ya maji, hii maana yake ni kwamba hatufanyi shughuli yoyote ya uzalishaji isipokuwa kila siku ni kuhangaika na maji,” amesema Agnes

“Huu mradi tunausubiri kwa hamu kubwa na tutaulinda kwasababu mama zetu, dada zetu na wake zetu wamekuwa wakihangaika mno kutafuta maji maana hapa tuna visima ambavyo vinakuwa na maji nyakati za mvua na mvua zikiisha tu ni mwendo wa ziwani, inachosha sana,” amesema Joshua Manyama

Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma,  Dk. Halfan Haule amesema mradi huo utatekelezwa kwa awamu ili kuweza kunufaisha vijiji zaidi ya sita katika halmashauri hiyo.

“Baada ya serikali kugundua hapa kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji basi ikaamua kuja na huu mradi ambao mbali na hivi vijiji vitatu vya mwanzo lakini pia utaboreshwa zaidi ili wenzenu wa vijiji vingine pia wapate maji safi na salama kwa uhakika,” amesema Dk. Haule

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!