Balozi wa Tanzania Nchini Algeria Imani Njalikai Leo Oktoba 26, 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kituo cha Uwekezaji na Maendeleo cha Waarabu wa Afrika (CAAID), Dkt. Amine Boutalbi, katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers.
Mheshimiwa Balozi Njalikai amesema kuwa ubalozi wa Tanzania Algiers utashirikiana na mamlaka za Tanzania hususan TPSF, TIC na TANTRADE kufanikisha ushiriki wa wafanyabiashara wa Tanzania kwenye makongamano ya uwekezaji na biashara yanayoandaliwa na Kituo cha CAAID mwezi Mei 2024.
Balozi Njalikai ameongeza kuwa watashirikiana na CAAID kuratibu kongamano maalumu la wafanyabishara wa Algeria nchini Tanzania mwaka 2024 kwa lengo kuimarisha uwekezaji na biashara kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Algeria.
Dkt. Boutalbi amemhakikishia Balozi Njalikai kuwa CAAID itaratibu ushiriki wa wafanyabiashara wa Algeria kwenye maonesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) maarufu Maonesho ya Saba Saba kwa mwaka 2024.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano na CAAID ambayo ni kiungo muhimu kati ya Ubalozi na Sekta Binafsi nchini Algeria katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.