Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango leo terehe 23 Oktoba 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika Mazungumzo hayo Makamu wa Rais amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo baina yake na Qatar na imedhamiria kuimarisha na kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya mataifa yote mawili. Makamu wa Rais ametaja maeneo yanayoweza kuongezwa ushirikiano baina ya Tanzania na Qatar ikiwemo sekta ya Afya, utafiti wa mafuta na gesi pamoja na biashara ikiwemo bidhaa zinazotokana na mafuta.
Hali kadhalika Makamu wa Rais ameikaribisha Qatar kuwekeza katika viwanda vya uzalishaji dawa na vifaa tiba pamoja na kushirikiana katika teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kuwasaidia wananchi kuondokana na matumizi ya kuni na mkaa na kuimarisha matumizi ya nishati mbadala. Pia amesema Qatar na Tanzania zinaweza kushirikiana kwenye utalii pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu ikiwemo wataalamu wa afya.
Kwa upande wake Balozi wa Qatar nchini Tanzania Mhe.Fahad Rashid Al-Muraikhi amesema Tanzania na Qatar zinapaswa kuongeza ushirikiano wake ili kuweza kutumia vema fursa zilizopo katika mataifa hayo. Balozi muraikhi ameahidi kufanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania ili kuongeza ushirikiano katika masuala ya kibiashara.
Kwa pamoja viongozi hao wamejadili namna ya kufanyika kwa ziara za wafanyabiashara na wawekezaji baina ya mataifa hayo mawili ambazo zitaweza kusaidia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali ikiwemo za afya, michezo na utamaduni.