Na Shomari Binda-Bunda
TIMU ya Amani FC na Kabasa FC kesho zinashuka kwenye dimba la Sabasaba mjini Bunda kutoana jasho kwenye robo fainali ya kwanza ya mashindano ya Ester Bulaya Cup 2023.
Mashabiki wa timu zote mbili wameendeleza tambo kwenye viunga mbalimbali vya mji wa Bunda huku kila upande ukitamba kushinda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mzawa Blog mashabiki hao wamesema itakuwa robo fainali ya ushindani kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri.
Juma Warioba aliyejitambulisha kama shabiki wa Amani amesema licha ya kujuana vizuri na Kabasa lakini wanakwenda kushinda mchezo huo.
Amesema wamejiandaa vizuri kwenda kupambana na wachezaji wao wamewahakikishia kuwapa burudani kwenye mchezo huo na kutinga nusu fainali.
Kwa upande wao mashabiki wa timu ya Kabasa wamesema hawana hofu na Amani kwa kuwa wanawamudu na wana uhakika wa kushinda mchezo huo.
Wamesema wanakiamini kikosi chao na mashindano ha mwaka huu watafika hatua ya fainali na kuchukua ubingwa na kwenda nao Kabasa.
Rekodi zinaonyesha timu hizo zinapokutana kwenye mashindano mbalimbali yanayofanyika mjini Bunda zimekuwa zikionyeshana upinzani.
Mashindano ya Ester Bulaya ya mwaka huu yamekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu kutokana na maandalizi waliyofanya kwa muda mrefu.