Home Kitaifa WAZIRI MAVUNDE ATOA ONYO WATOROSHAJI MADINI NCHINI

WAZIRI MAVUNDE ATOA ONYO WATOROSHAJI MADINI NCHINI

Utoroshaji Madini kunaikosesha Serikali Mapato

Aeleza zaidi ya Kilogram 4 za madini zilikamatwa Kahama

Serikali imewataka wadau wote wa Sekta ya Madini nchini kutojihusisha na vitendo vya utoroshaji madini katika maeneo yoyote yenye uchimbaji, uhifadhi na uuzaji kwani kwa kufanya hivyo kunaikosesha Serikali kupata mapato yatokanayo na rasilimali madini.

Hayo yalibainishwa jana Oktoba 19, 2023 na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akizungumza na Wanachama wa Chama cha Mabroka Tanzania (CHAMMATA) jijini Dodoma.

Mhe. Mavunde amesema kuwa Serikali ina mipango mingi katika kuendeleza Sekta ya Madini lengo likiwa ifikapo mwaka 2025 sekta hii kuchangia asilimia zaidi ya kumi (10%) katika pato la Taifa (GDP) kama mpango wa Maendeleo wa Dira ya Taifa 2025 unavyoelekeza.

Akielezea kuhusu mchango wa madini katika Pato la Taifa, Mhe. Mavunde amefafanua kuwa katika Mwaka 2022/2023 Sekta ya Madini ilikusanya zaidi ya shilingi Bilioni 600 huku asilimia 40 ikichangiwa na wachimbaji wadogo , wafanyabiashara wa madini wa ndani na Broka.

Akielezea kuhusu mzunguko wa fedha katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini , Mhe. Mavunde amesema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliweza kukusanya mapato ya kodi ya ndani ya kiasi cha shilingi trilioni mbili kulingana na mzunguko wa fedha katika masoko ya ndani ya madini.

Naye, Mwenyekiti wa CHAMMATA Jeremia Kituyo ameshauri kuwa ili kuondokana na utoroshaji wa madini nchini ni vyema Serikali ikaja na mpango wa kukata leseni kwa mfumo wa kikanda ili kutoa wigo mpana kwa wafanyabiashara kutoka kanda moja na nyingine.

Kituyo ameongeza kuwa ni muda muafaka wa Serikali kuweka biashara ya madini kuwa huria katika masoko ya madini hususan katika minada ili kuwezesha bei kuwa shindani katika masoko ya madini.

Akielezea kuhusu lengo la kuanzishwa kwa CHAMMATA Kituyo amefafanua kuwa ni pamoja na kuwaunganisha wafanyabiashara wa madini na Serikali pamoja na kutetea na kusimamia haki za wafanyabiashara wa madini nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!