NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amesema kuwa miaka mitatu ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi,inaiweka Zanzibar katika orodha ya nchi za visiwa zinazoendelea kwa kasi kubwa kiuchumi.
Hayo ameyasema wakati akizindua bonanza la kupongeza miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Mwinyi,lililoandaliwa na Mwakilishi wa Jimbo la Chwaka Mhe.Ussi Haji Gavu kwa kushirikiana na UVCCM Wilaya ya Kati Unguja, katika Chwaka.
Mbeto, alisema maendeleo yaliyofikiwa hivi sasa nchini katika nyanja za kiuchumi,kisiasa na kijamii ni kielelezo cha kujivunia utawala bora unaofuata sheria,utu na haki za binadamu unaosimamiwa na Serikali ya awamu ya nane chini ya Uongozi wa Dk.Mwinyi.
Alifafanua kwamba mafanikio hayo katika sekta za elimu,afya,kilimo,maji safi na salama,miundombinu ya usafiri wa anga,majini na nchi kavu sambamba na ujenzi wa barabara za kisasa mijini na vijijini vinatakiwa kulindwa na kuthamini ili viwe na manufaa kwa wananchi wote.
“Dhamira ya bonanza hili ni kupongeza miaka mitatu ya uongozi wa Rais wetu Dk.Hussein Mwinyi, amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo hapa nchini kila mwananchi ananufaika kwa namna yake, tuendelee kumuunga mkono na kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kudumu.”alisema Mbeto.
Katika maelezo yake Katibu huyo wa NEC Zanzibar Mbeto, alisema ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Dk.Mwinyi, tayari Serikali imevuka malengo ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Kupitia bonanza hilo aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt.Samia Suluhu Hassan, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Hussein Ali, Mwinyi kwa kasi yao kubwa ya kiutendaji inayotoa muelekeo wa kupatikana kwa ushindi mkubwa wa Dola mwaka 2025.
Bonanza hilo limejumuisha mashindano ya mbio za Baiskeli pamoja na mbio za Ngalawa ambapo washindi wa mashindano hayo wamekabidhiwa zawadi mbalimbali.