Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini profesa Sospeter Muhongo amesema katika kumuenzi Baba wa Taifa ni kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Amesema enzi ya uhai wake Mwalimu Nyerere amekuwa akisisitiza kilimo hususani cha umwagiliaj ili kupata mazao yenye tija.
Muhongo amesema oktoba 14, 2023 inakumbusha mengi ambayo Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyafanya kwa lengo kuu la kuboresha uchumi na ustawi mzuri wa Taifa.
Amesema alithamini sana kilimo na kuwekeza kwenye viwanda vya zana za kilimo kama UFI, kiwanda cha mbolea, viwanda vya kutumia mazao ya kilimo na ufugaji, vyuo vya kuzalisha wataalamu wa kilimo wa ngazi mbalimbali, vyama vya ushirika, ushirikiano na nchi za nje kwenye sekta ya kilimo, JKT yenye mashamba ya kilimo, tuzo na sherehe za wakulima.
Mbunge huyo amesema Baba wa Taifa alipeleka nje ya nchi vijana wa kitanzania kusomea masuala mbalimbali ya kilimo, ufugaji na uvuvi.
Vilevile Baba wa Taifa aliamua kuwekeza kwenye kilimo kikubwa cha umwagiliaji na moja ya miradi hiyo ni ule wa bonde la Bugwema la Musoma Vijijini.
Amesema serikali imeamua kufufua mradi wa Bugwema ambao miundombinu ya umwagiliaji ilianza kujengwa mwaka 1974. Mradi ukasimama.
‘”Katika kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ni muhimu kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji kwenye maeneo mbalimbali”
“Tunaishukuru serikali yetu imeanza kutenga fedha kwaajili ya kilimo cha umwagiliaji kwenye shamba la Bugwema” amesema Muhongo.