Home Kitaifa SACP Mutafungwa: Ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi

SACP Mutafungwa: Ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbrod Mutafungwa amewataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika suala la ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo vya uhalifu.

Hayo yamejiri jana Oktoba 10,2023 wakati wa mkutano wa hadhara na wananchi pamoja na viongozi wa serikali za mtaa wa kata ya Pamba wilaya ya Nyamagana Jijini Mwanza wakati akisikiliza kero mbalimbali za kiusalama kutoka kwa wananchi hao.

Kupitia mkutano huo wananchi waliwasilisha kero na changamoto wanazokutana nazo eneo hilo ikiwemo viongozi na wazazi kushirikiana na wahalifu kwa kuwaficha baada ya kufanya uhalifu.

Akijibu kero mbalimbali kutoka kwa wananchi hao kamanda Mutafungwa amewataka wananchi kutambua kuwa suala la ulinzi na usalama ni jukumu la kila mwananchi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi huku wakitoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Sahara Mussa Hassan kupitia mkutano huo aliwasilisha malalamiko yake kuwa wananchi wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha kwa vikundi vya ulinzi shirikishi.

”Ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wananchi umekuwa ni mdogo sana, kama unavyofahamu suala la ulinzi ni mtambuka lakini hakuna ushirikiano” alisema Hussen

Hata hivyo kamanda Mutafungwa aliwataka viongozi wa serikali za mitaa kutokumbatia vitendo vya uhalifu badala yake washirikiane na mkaguzi kata wa kata hiyo kuboresha vikundi vya ulinzi shirikishi vitakavyosaidia kudhibiti uhalifu. Pia, aliwasisitiza wazazi na walezi kuwa na malezi bora kwa watoto wao kwani wamekuwa wakijiingiza kwenye dimbwi la uhalifu ambao unawapelekea kufifisha ndoto zao za baadae.

”Kwanini tunawaacha watoto hadi utoro unaongezeka, wanaingia mtaani wanageuka wanakuwa waporaji nikuagize mkaguzi wa kata kesho ukutane na walimu pamoja na wazazi wa watoto wanaorandaranda humu uongee nao tujue wapi kuna tatizo”

Baada ya kikao hicho Kamanda Mutafungwa ametangaza Operesheni kali ya kuwasaka wahalifu katika kata hiyo huku akitahadharisha wanaofanya hivo kuacha mara moja.

‘OCD yuko hapa, mkuu wa kituo yuko hapa kuanzia muda huu natangaza oparesheni kali, yaani nikigeuza tu gari yangu basi mjue kumekucha, wale ambao mmeshindikana niwaombe mjirekebishe kwasababu oparesheni hii haitaangalia wewe ni nani’ amesema Mutafungwa

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!