Home Kitaifa BMH KUFANYA UPASUAJI KUFUNGUA KIFUA WATU WAZIMA IKITIMIZA MIAKA 8

BMH KUFANYA UPASUAJI KUFUNGUA KIFUA WATU WAZIMA IKITIMIZA MIAKA 8

Oktoba 10, 2023 Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma itafanya upasuaji wa kufungua kifua kwa watu wazima kuanzia Oktoba 16 mwaka huu.

Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Alphonce Chandika alipokuwa akitoa taarifa ya miaka 8 ya mafanikio ya utoaji wa Huduma za Kibingwa na Ubingwa bobezi mapema leo.

“Hii ni hatua kubwa kwetu, kwa kuwa tumekuwa tukitoa huduma hizo kwa Watoto pekee, hivyo tutashirikiana na wenzetu wa JKCI ili kusogeza huduma hizo kwa wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wa Moyo nchini” Alisema Dkt. Chandika

Aidha, ametumia mkutano wake huo na waandhishi wa Habari kuishukuru Serikali kwa kuwekeza vifaa tiba vya kisasa vinavyoiwezesha Hospitali yake kuokoa Maisha ya wananchi na kuwapunguzia mzigo wa gharama za kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu ya kibingwa.

Akifafanua kuhusua mafanikio ya Hospitali hiyo, amesema kuwa Hospitali hiyo inaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwekeza katika vifaa tiba vya kisasa.

“Kwa miaka hii nane serikali imesimika vifaa vya kisasa ikiwemo Laser lithotripsy, inayoweza kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo na Figo kwa kutumia mawimbi ya sauti na kumsaidia mgonjwa kutolazwa, kutokuwa na jeraha, na kutumia gharama ndogo kutibiwa ikilinganishwa na upasuaji wa kawaida” Alisema Dkt. Chandika.

Akitaja mashine nyingine Dkt. Chandika alisema kuwa Maabara ya Uchunguzi na matibabu ya Moyo Cath-lab, iliyopo hospitalini hapo imeokoa Maisha ya mamia ya watanzania hasa wanaokabiliwana magonjwa ya Moyo.

“Bila kuwepo mashine hiyo, kuna wagonjwa wasingeweza kufika Dar es Saalam hasa wale wanaokabiliwa na shambulio la Moyo kwa kuziba mishipa ya damu” Aliongeza Dkt. Chandika.

Mbali na uwekezaji wa mashine alisema uwekezaji miundombinu, rasilimali watu unaofanywa na serikali ya awamu ya sita umeiwezesha Hospitali ya Benjamin Mkapa kuwa ya kwanza nchini, Afrika Mashariki na Kati kutoa huduma za upandikizaji wa uloto kutibu seli mundu.

“Nyote mtakumbuka mwezi wa tano, Mheshimiwa Kassimu Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania, alikuja kuzindua huduma za upandikizaji wa uloto, huduma inayoleta unafuu kwa Watoto wenye Sickle Cell na familia zao, ndiyo maana pamoja na Uchanga wetu tumepokea tuzo ya Daktari wa mwaka Dkt. Stella Malangae, anayesimamia huduma za Upandikizaji wa Uloto” alisema Dkt. Chandika.

Huduma nyingine za kibingwa na ubingwa bobezi zilizoweza kuanzishwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa ni pamoja na Upandikizaji wa Figo, Matibabu ya Mifumo ya Fahamu, Uti wa Mgongo na Ugongo, Upasuaji wa kubadili nyonga na Magodi kwa kuweka vipandikizi na Kuweka Betri kwenye Moyo.

“lengo letu ni kuhakikisha tunatumia kila sayansi ya inayopatikana duniani kutoa na kuokoa Maisha ya watanzania” Alisisitiza Dkt. Chandika.

Oktober 13, Hospitali ya Benjamin Mkapa itatimiza miaka 8 ya huduma tangu ilipozinduliwa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu nne, tangu wakati huo imekuwa muhimili wa matibabu kwa wakaazi wa mikoa ya kanda ya kati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!