Na Shomari Binda-Musoma
JESHI la polisi mkoani Mara limewataka vijana kuitumia michezo kuinua vipaji vyao na kutojiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Opateshini wa Jeshi la Polisi mkoani Mara, ACP Mahamoud Banga kwenye mchezo wa kutafuta mshindi wa 3 wa mashindano hayo uliofanyika kwenye uwanja wa Mara sekondari.
Amesema michezo imekuwa ikiinua vipaji na kuzalisha ajira na imekuwa ikiwapa mafanikio makubwa na kuwapa kipato washiriki.
Banga amesema uhalifu na wahalifu utakomeshwa iwapo kutakuwa na ushorikiano wa kila mmoja na sio kuachia jeshi la polisi pekee.
Amesema utoaji wa taarifa ni muhimu katika kupambana na uhalifu na wahalifu huku akitoa wito kwa jamii kulipa ushirikiano jeshi la polisi.
Mkuu huyo wa oparesheni wa jeshi la polisi mkoa wa Mara amesema hali ya usalama mkoani Mara ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea kushiriki michezo na kufanya kazi halali za kuwaingizia kipato.
Aidha amemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo kwa kuanzisha mashindano hayo ambayo yanawakutanisha wananchi na wao kuwapa elimu ya kuzuia uhalifu.
Katika mchezo huo wa kutafuta mshindi wa 3 timu ya Makoko imechomoza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nyakato fc.
Fainali ya mashindano hayo ya Mathayo Cup 2023 yatahitimishwa siku ya jumamosi kwa mchezo dhidi ya Mwigobero fc na Nyamatare fc huku ikitanguliwa na michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa mashabiki veteran wa Simba na Yanga na kutolewa zawadi mbalimbali.