Na Dorina Makaya & Issa Sabuni
Naibu Waziri wa Nishati Mheshimiwa Judith Kapinga amesema, Miradi yote ya Nishati kuanzia sasa itasimamiwa kwa jicho la ukaribu zaidi ili kuhakikisha inatekelezwa ipasavyo na kwa wakati.
Naibu Waziri Judith Kapinga ameyasema hayo hivi Karibuni alipokuwa katika Hafla ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Namikunda kilichopo Wilayani Masasi, Mkoani Mtwara.
Amesema, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bilioni 97 kwa ajili ya Miradi ya kusambaza umeme Mkoani Mtwara.
Naibu Waziri Judith Kapinga amesema, fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuleta tija kwa maendeleo ya wananchi mmoja mmoja na Taifa zima kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa, azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara vinapatiwa umeme ili kuchagiza shughuli za Maendeleo na za Kijamii ni lazima itimie.
Naibu Waziri Kapinga ameongeza kuwa, Wizara ya Nishati, chini ya uongozi wa Dkt. Doto Biteko, itahakikisha fedha zote zinazotolewa na Serikali kwa Miradi yote ya Nishati nchini zinatumika ipasavyo.
Naibu Waziri Judith Kapinga, amewahamasisha wananchi wa Namikunda kutumia fursa ya uwepo wa Nishati ya Umeme Kijijini hapo kujiunganishia umeme na kuutumia katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kujiletea maendeleo.