Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Septemba 24, 2024 ametembelea Soko la Kimataifa la mazao ya Uvuvi la Katembe-Magarini lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera.
Akizungumza na wakazi wa eneo hilo Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imeweka utaratibu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuwawezesha wavuvi kufanya shughuli zao kwa tija.
Amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameweka nguvu ili kuwanufaisha wavuvi ikiwemo kununua boti kwa ajili ya vikundi vya wavuvi.
Pia Amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba kuhakikisha anaweka utaratibu mzuri wa uendeshaji wa Soko hilo ikiwemo kuajiri mtumishi wa Serikali badala ya kutoa ajira kwa vibarua
“Lete afisa mapato hapa, eneo hili litawasaidia kupata mapato mengi ambayo yatasaidia kuendesha soko hili ikiwemo kuweka taa za barabarani, Wavuvi wahudumiwe na wasaidiwe ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi”
Katika Mwaka fedha 2022/2023 Soko hilo linalohudumiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Halmashauri ya Muleba lilizalisha mazao ya Uvuvi ambayo ni Dagaa na Samaki tani milioni 26.96 kutoka visiwa vya Bumbire, Maziga, Ikuza, Kerebe na Goziba.
Katika Hatua nyingine Waziri Mkuu amemuelekeza Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Bandari Tanzania afanye maboresho ya bandari ya Magarini kwenye eneo la jengo la abiria na gati.