Home Kitaifa PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI KUWAVUSHA VIJANA

PROGRAMU YA KUENDELEZA KILIMO NA UVUVI KUWAVUSHA VIJANA

NA. MWANDISHI WETU

Imeelezwa kuwa, uwepo wa Programu ya Kuendelea Sekta ya kilimo na Uvuvi ya AFDP itasaidia kuwezesha jamii kwa kupewa elimu juu ya ufugaji wa Samaki kwa njia ya kisasa huku ikiwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo kwa vitendo.

Hayo yamelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga wakati wa ziara yake ya kikazi kufuatili shughuli za utekelezaji wa Program hiyo, ambapo alitembelea katika Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro amesema, Ofisi yake inajukumu kubwa na kuratibu program hiyo.

Naibu Waziri alisema, uwepo wa programu hiyo unatoa fursa kwa kundi la vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo kwa vitendo yanayotolewa na kituo hicho huku akiwaasa kuzingatia elimu wanayopata na kujali muda wanaoutumia ili kuwa na matokeo tarajiwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa program ya AFDP katika kituo, Kaimu Mkuu wa Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira Bi. Gilness Frank amepongeza juhudi za Serikali kwa kuendelea kuratibu uwepo wa program hiyo, huku akishukuru ufadhili wa Mfuko wa Kimataifa wa Kuendeleza Kilimo (IFAD) ambapo sekta ya uvuvi ni mnufaika.

“Programu hii imeendelea kuwa na tija kwetu tunaishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kufanikisha majukumu yake, imeendelea kuleta chachu kwa kuongeza uzalishaji wa Samaki, ajira katika mnyororo wa thamani na kuchangia kwenye uchumi pamoja na Tasnia ya ukuzaji viumbe maji nchini kukua,” alisema Bi. Gilness

Aliongezea kuwa kituo hicho kimeendelea kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma za ugani na mafunzo kwa vitendo kwa wanavyuo na watafiti kutoka Taasisi za ndani na Nje ya nchi.

“Wadau wengi wamekuwa wakifika kituoni hapa kujifunza njia na kanuni bora za ufugaji wa Samaki, kupata vifaranga bora vya Samaki pamoja na kupata wataalam wa kutengeneza vyakula vya Samaki.

Alifafanua kuwa, jumla ya wafugaji 1319 wamenufaika kwa kupatiwa elimu ya ukuzaji viumbe maji, aidha jumla ya vifaranga 340630 aina ya sato vilizalishwa na kuwezesha kukusanya maduhuli jumla ya shilingi milioni 26, 171,000.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitengo katika kituo hicho, Afisa Uvuvi wa kituo Bw. Ali Issa alipongeza ujio wa Naibu Waziri huo na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendelea kujali na kuwezesha shughuli za uzalishaji zinazoendelea kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zao.

“Kipekee nakushukuru sana kwa niaba ya vijana wenzangu, tunaahidi kuendelea kuwapa ujuzi vijana hawa ili wajifunze na kuleta tija katika sekta ya uvuvi nchini,” alisisitiza Ali.

=MWISHO=

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!