Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Eng. Rogatus H. Matavila amesema Mradi wa Bonde la Mto Msimbazi ukikamilika utalibadilisha na Kulipendezesha Jiji la Dar es Salaam
Ameyasema hayo leo alipofanya Ziara katika Ofisi za Kikundi-kazi cha Utekelezaji wa Miradi inayotekelezwa kwa Ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI na Benki ya Dunia kupitia TARURA, Jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Miradi hiyo Mhandisi Humprey Kanyenye amemueleza kuwa Kikundi-kazi hicho kwa sasa Kinasimamia utekelezaji wa Mradi wa Uendelezaji wa Miji Tanzania (TACTIC) wenye lengo la kuboresha Miundombinu ya Miji 45 ya Tanzania.
Pia Kinasimamia Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi wenye lengo la kukabiliana na Mafuriko katika Bonde la Msimbazi na kuboresha matumizi ya Ardhi katika eneo la chini ya Bonde.
Kikundi-kazi hicho Pia Kinasimamia mradi wa DMDP Awamu ya Pili ambao ni mwendelezo wa kazi nzuri iliyofanyika Awamu ya kwanza ya mradi huo na utazinufaisha Halmashauri zote tano za Jiji la Dar es Salaam.
Katika Ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu Matavila amekutana na kufanya kikao Kazi na Watumishi wa Kikundi-kazi hicho na kutembelea Maeneo yatakayopitiwa na Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi.