Na Shomari Binda-Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amepongeza jitihada za mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara Agness Marwa kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Kauli hiyo ameitoa mjini Musoma wakati mbunge huyo akichangia vikundi vya wanawake wa Kata ya Iringo vifaa mbalimbali vya ujasiliamali vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.
Amesema amekuwa akiona na kusikia taarifa mbalimbali za mbunge huyo akichangia shughuli za kiuchumi maeneo mbalimbali.
Mtanda amesema suala la kujitoa na kuchangia ni suala la moyo na mbunge Agness amekuwa akifanya hivyo kila wakati.
Mkuu huyo wa mkoa amewataka wanawake waliowezeshwa vifaa hivyo kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kujiinua kiuchumi.
“Mheshimiwa Agness amekuwa akijitoa katika kuchangia shughuli za maendeleo hasa kwa wanawake hivyo ni muhimu kumpa ushirikiano”, amesema Rc Mtanda.
Akikabidhi vifaa hivyo kwenye vikundi vya wajasiliamali wa Kata ya Iringo manispaa ya Musoma,mbunge wa viti maalum mkoa wa Mara,Agness Marwa amesema ataendelea kuwa pamoja na wanawake bega kwa bega katika kusaidiana kujiinua kiuchumi.
Amesema yeye ametokea kwenye ujasiliamali hivyo hawezi kuwaacha kila atakapopata nafasi na kuwataka kuendelea kumsemea Rais Samia kwa mazuri anayolifanyia taifa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Mara Nancy Msafiri amempongeza mbunge Agness kwa kazi nzuri anayoifanya kupitia nafasi yake.
Viongozi wa vikundi vya wanawake wajasiliamali hao wameshukuru vifaa walivyopata kuwa vinakwenda kuwainua kiuchumi.