Amepokea Vitabu vya Madini yapatikanayo Tanzania kwa shangwe
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas ametoa wito kwa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufungua tawi katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Makaa ya Mawe ikiwemo Mkoa wa Ruvuma.
Kanal Thomas ameyasema hayo Ofisini kwake wakati akipokea toleo la Vitabu vipya vinavyoonesha Madini yapatikanayo Tanzania vya Mwaka 2023 vilivyoandaliwa na GST.
Amesema uzalishaji wa Makaa ya Mawe unafanyika kwa kiwango kikubwa mkoani humo ambapo wafanyabiashara wanatumia mianya ya kuto kuwa na maabara ya kutambua ubora wa Makaa hayo kupunguza bei ya bidhaa hiyo, hivyo ameiomba GST kusogeza huduma hiyo ili kuwapunguzia adha ya kusafirisha sampuli kupeleka nje ya nchi kwa ajili ya vipimo.
Aidha, amesema ameuongoza Mkoa huo kwa muda mrefu na hakuwahi kujua kuwa Mkoa huo una Madini mengi mbali na yale waliyozoea kuona yanavunwa ambapo ameahidi kusambaza taarifa za Madini yapatikanayo Mkoani humo kwa wadau mbalimbali pamoja na kuhuisha taarifa za madini kwenye tovuti (Website) ya Mkoa kwa lengo la kutafuta Wawekezaji.
Kwa upande wake, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Solomon Maswi amesema, jukumu kubwa la GST ni kufanya tafiti za madini, kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusiana na madini na kuratibu majanga ya asili ya jiolojia.
“Leo tumekuja ofisini kwako mahususi kukukabidhi Vitabu vya Madini yapatikanayo Tanzania ili uweze kujua rasilimali zilizopo mkoani kwako ambalo ni agizo la Waziri Mkuu ili kuvutia uwekezaji mkubwa katika eneo lako,” amesema Maswi.
Pamoja na Mambo mengine, Maswi amesema Mkoa wa Ruvuma una madini mbalimbali tofauti na wadau wajuavyo kuwa ni Makaa ya mawe, urani na vito pekee, hivyo Kitabu hicho kinaonesha Madini hayo katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata mpaka Kijiji na hivyo kitasaidia kwa kiwango kikubwa kuhamasisha Wawekezaji kuja kufanya utafiti wa kina.