DADA wa kazi za ndani Filomena Erick (17) amejeruhiwa na mwajiri wake Janeth Dominick (26) kwa kumwagia chai ya moto kwa tuhuma za kuiba simu, sukari na unga kwa jirani huko Kibaha kwa Mathias.
Aidha mtuhumiwa huyo anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kwa tuhuma hizo za tukio la kudhuru mwili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mjini Kibaha na Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Pius Lutumo imesema kuwa mtuhumiwa alimuunguza mlalamikaji sehemu mbalimbali za mwili.
Tukio hilo limetokea Septemba 14 2023 majira ya saa 2:00 asubuhi ambapo mtuhumiwa alimuunguza maeneo ya shingoni, mkononi, kifuani na tumboni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtuhumiwa alifikia hatua hiyo kwa kumtuhumu kuiba unga, sukari na simu ya mkononi katika chumba cha mpangaji mwenzao.
Mtuhumiwa atafikishwa kwenye mifumo ya kisheria mara upelelezi utakapokamilika kuhusiana na tukio hilo.