Na Shomari Binda-Musoma
KUELEKEA maadhimisho ya miaka 23 ya Mwalimu Nyerere, taasisi ya kumbukumbu ya Mwl. Nyerere Mkoa wa Mara imekusudia kufungua klabu za Mwalimu Nyerere mashuleni.
Lengo za klabu hizo ni kuwafanya wanafunzi kukutana na kumzungumzia farsafa zake ikiwemo uzalendo na mapambano dhidi ya Rushwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa taasisi hiyo mkoa wa Mara, Emmanuel Masse alipokuwa akizungumza na Mzawa Blog.
Amesema bila kuweka misingi mizuri ya wanafunzi kumzungumzia Mwalimu Nyerere wengi wao hawatazielewa farsafa zake.
Masse amesema wanataraji kuzifikia taasisi zote za elimu ili kuzifungua klabu hizo kuwafanya kukutana kiurahisi.
Amesema kwenye klabu hizo watakuwa wakizungumzia masuala ya uzalendo na mapambano dhidi ya Rushwa.
“Ni muhimu kuweka misingi mizuri kwa wanafunzi kumzungumzia Mwalimu Nyerere hususani farsafa zake”
“Uzalendo pamoja na mapambano dhidi ya Rushwa ni mambo ambayo tumelenga wanafunzi wayapate kupitia klabu hizi” amesema Masse.
Katibu huyo amesema wanatarajia pia kufanya mikutano na makongamano ya kukutana na wananchi ili kuitambulisha taasisi hiyo na majukumu wanayofanya.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere hufanyika kila mwaka oktoba 14 kwa kufanyika makongamano mbalimbali ya kumzungumzia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.