Na Shomari Binda-Serengeti
MAKAMU Mwenyekiti wa Halmashauri ya Serengeti, Samson Ryoba, ameahidi ushirikiano kwa madiwani ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Kauli hiyo ameitoa baada ya kuchaguliwa kwa kipindi cha tatu kuwa Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.
Ryoba ambaye pia ni diwani wa Kata ya Kisangura amesema imani ambayo madiwani wamemuonyesha ni Kubwa kwake katika kipindi kingine.
Makamu Mwenyekiti huyo amesema katika vipindi vilivyopita alipata ushirikiano wa kutosha na kuamini kuendelea kupewa ushirikiano.
Amesema wananchi wa Serengeti pia wanayo matumaini na madiwani kwenye Kata hivyo ni muhimu kupata ushirikiano kutoka kwenye halmashauri.
“Nawashukuru waheshimiwa madiwani kwa kuendelea kuonyesha imani kwangu na kunichagua tena kwenye nafasi hii.
“Nimekuwa nikishirikiana nanyi pamoja na Mwenyekiti ili kusukuma mbele maendeleo ya wananchi wetu na kuisimamia vyema halmashauri.
“Wananchi wanatutegemea kwenye Kata zetu ili kusukuma maendeleo ni vyema tushirikiane kwa pamoja kwenye kila jambo la kimaendeleo“,amesema Ryoba.
Amesema ushirikiano kutoka kwa mkurugenzi na watumishi wa halmashauri wamekuwa wakiutoa kwa karibu hali inayopelekea kuchochea maendeleo.