Na Shomari Binda-Musoma
TIMU ya Kitaji fc imekuwa ya kwanza kutinga hatua ya 8 bora ya mashindano ya Mathayo Cup huku Iringo fc ikitupwa nje ya mashindano hayo.
Kitaji imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga timu ya Mwigobero mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika uwanja wa Posta majira ya saa 8 mchana.
Kwa matokeo ya leo Kitaji fc wamefikisha point 6 na mabao 6 ya kufunga kutoka kundi A huku ikiwa imebakiza mchezo mmoja dhidi ya Mukendo.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo timu ya Iringo fc imeaga rasmi mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha pili mfululizo cha mabao 4-1 kutoka kwa Mukendo fc.
Diwani wa Kata ya Mukendo,Abasi Chamba,amesema baada ya matokeo ya leo wanakwenda kuiandaa timu ili waweze kupata matokeo dhidi ya Kitaji ili waweze kutinga rasmi hatua ya 8 bora.
Amesema kama timu yake itacheza dhidi ya Kitaji kama ilivyocheza leo watakwenda kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa mwisho.
“Vijana wangu wamecheza vizuri kwenye mchezo wa leo dhidi ya Iringo nawapongeza sana na wakienda kucheza hivi mchezo wa mwisho tutashinda tena.
“Mukendo inavyo vipaji vya kutosha na ni imani yangu msimu huu katika mashindano haya ya Mathayo Cup tunakwenda kuchukua ubingwa”,amesema Chamba.
Kesho mashindano hayo yanayovutia wakazi wa mji wa Musoma yataendelea tena kwenye uwanja wa Buhare chuoni ambapo katika mchezo wa mapema majira ya saa 8 mchana timu ya Makoko fc itakutana na Buhare fc huku Kamnyonge ikiumana na Mwisenge fc