Na Shomari Binda-Serengeti
CHAMA cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Serengeti kimewapongeza madiwani wa halmashauri hiyo kwa kusimamia miradi ya maendeleo kwenye Kata zao.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Japan Mrobanda alipokuwa akitoa salam kwenye kikao cha kawaida cha robo ya 4 cha baraza la madiwani.
Amesema kama wasimamizi wa ilani ya uchaguzi inayotekelezwa wanalidhishwa na kazi inayofanywa na madiwani.
Mrobanda amesema Kata zote 30 ipo miradi inayoendelea ikiwemo ya elimu, afya, maji na miundombinu inayoendelea na inasimamiwa vizuri.
Amesema serikali ya awamu ya 6 chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan,imekuwa ikitoa fedha nyingi za miradi na madiwani wamekuwa wakiisimamia vizuri.
“Niwashukuru na kuwapongeza sana madiwani kwa kazi nzuri mnayoifanya kwenye Kata zenu na halmashauri yetu ya Serengeti”
“Muendelee kutekeleza majukumu yenu na naamini nawaombea kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 mtarudi kwenye nafasi zenu” ,amesema Mrubanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti,Ayub Mwita Makuruma,ametoa wito kwa kila kiongozi kwenye eneo lake kutimiza wajibu wake ili kumsaidia kazi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema fedha za miradi zinakuja kinachotakiwa ni uwajibikaji ukiwemo usimamizi ili kuweza kuwaletea wananchi maendeleo na kuwataka viongozi wa taasisi kutimiza wajibu wao na kutoa ushirikiano kwa madiwani.
Katika baraza hilo madiwani hao wamezitaka taasisi zinazofanya kazi kwenye halmashauri hiyo zikiwemo za Ruwasa, Tarura, Muwasa, Tanesco na nyinginezo kutimiza wajibu wao.
Wamesema kama wasipotekeleza ipasavyo majukumu yao watakipa wakati mgumu chama cha mapinduzi katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2024.