Home Kitaifa Kampeni ya Kili Challenge 2023 kuchochea malengo ya kuzifikia SIFURI TATU-WAZIRI MHAGAMA

Kampeni ya Kili Challenge 2023 kuchochea malengo ya kuzifikia SIFURI TATU-WAZIRI MHAGAMA

Na Mathias Canal, Moshi-Kilimanjaro

Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI ambapo mwaka huu mpya wa fedha wa 2023/2024 zimetengwa fedha nyingi zaidi kuhakikisha kila Wizara na Taasisi ya Umma zinawezeshwa katika mapambano hayo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama leo tarehe 20 Julai 2023 Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuwapoke Mashujaa waliojitolea kupanda Mlima Kilimanjaro na wengine kuuzunguka kwa baiskeli ili kuchangisha fedha kwa ajili ya kuchangia juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.

Serikali iliweka Lengo A (objective A) ambalo kila Wizara na Taasisi ya Umma zinatakiwa kutenga fedha kwa ajili ya masuala ya VVU na UKIMWI. Katika mwaka 2022/23, Serikali ilitenga shilingi bilioni 41 na mwaka 2023/24 imeweka fedha zaidi,” alieleza

Aidha, licha ya fedha zilizo katika Lengo A, katika mwaka 2022/23, TACAIDS ilitengewa shilingi bilioni 14.98 kwa ajili ya masuala ya VVU na UKIMWI pekee na mwaka 2023/24 zimetengwa shilingi bilioni 25.86 ikiwa na lengo la kuendeleza mapambano hayo.

Pamoja na hilo TACAIDS imeendelea kuufikia umma wa Watanzania kupitia program mbalimbali ikiwemo mafunzo na kutoa miongozo juu ya mapambano haya.

Tumeendelea kutoa miongozo ya kudhibiti VVU na UKIMWI pamoja na Magonjwa sugu yasiyoambukizwa ili kuhakikisha jamii inapata elimu kuhusu masuala haya na kupinga unyanyapaa” Amekaririwa Mhe Mhagama.

Amesema kuwa, ili kuzifikia SIFURI TATU kutokuwa na Maambukizi Mapya, Kutokuwa na Unyanyapaa na Ubaguzi, na Kutokuwa na Vifo Vitokanavyo na UKIMWI, ambapo amesema ipo haja ya kuendelea kuunga mkono jitihada hizo kupitia Kuchangia Mfuko wa Kili Challenge ili kuwa na matokeo yanayotarajiwa.

Kwenye Kampeni ya Killi Challenge jumla ya shilingi milioni 543 ziligawiwa kwa Halmashauri zinazohudumia Konga nchini ili kuwasaidia katika shughuli zao.

Waziri Mhagama ameushukuru uongozi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) pamoja na wadau mbalimbali katika kuandaa na kuwezesha Kampeni ya Kilimanjaro Challenge against HIV and AID” kufanyika kila mwaka na kutambua jitihada zinazofanywa na Uongozi wa Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Geita bila kusahau Sekretarieti za Wilaya za Hai na Moshi kwa kuratibu na kuwa wenyeji wa tukio hilo kila mwaka.

Aidha aliwapongeza mashujaa walioshiriki katika kampeni hiyo na kutoa rai kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi mwaka ujao katika Kampeni ya Kili Challenge.

Hivyo, kwa moyo dhati kabisa, tunawapongeza mashujaa wote (61) ambapo 35 mlipanda Mlima na 26 mliendesha baiskeli kuzunguka Mlima huo kwa mafanikio mliofikia. Mafanikio yenu yanadhihirisha kuwa mwitikio dhidi ya VVU na UKIMWI unawezekana iwapo kutakuwa na dhamira ya dhati kwa kila mmoja wetu na ushirikiano wa pamoja wa kufikia Malengo ya kitaifa,” alisisitiza Mhe. Mhagama

=MWISHO=

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!