Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma Mjini Vedastus Mathayo amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Musoma kufungua na kuzifanya barabara kupitika.
Kauli hiyo ameitoa leo alipotembelea ofisi za TARURA kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
Amesema kutokana na taarifa ya utekelezaji wa miradi na namna alivyoziona barabara amelidhika na kazi iliyofanywa.
Mathayo amesema katika kipindi cha nyuma barabara nyingi hususani za pembezoni zilikuwa hazipitiki lakini leo hii nyingi zimefunguliwa.
Amesema katika maeneo ya Bweri Bukoba, Nyabisare, Majenngo hadi Nyamiongo-Zanzibar kulikokuwa na tatizo la barabara sasa kunapitika.
Mathayo amesema katika utekelezaji wa miradi awamu inayofuata ni kuhakikisha maeneo yote korofi yanaingizwa kwenye miradi.
“Niwashukuru sana na kuwapongeza Tarura wilaya ya Musoma kwa kazi nzuri mnayoifanya,Mhandisi Mkwizu na timu yako yote”
“Leo wananchi wa pembezoni kulikokuwa na shida ya kufika majumbani wanafika na niwaombe muendelee na kasi hiyo mliyonayo”
Aidha mbunge Mathayo ameishukuru serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi jimbo la Musoma mjini kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake meneja wa TARURA wilaya ya Musoma mhandisi Joseph Mkwizu amesema wataendelea kufanya kazi kwa weledi kwa kila fedha wanayopokea kwaajili ya miradi ya barabara.