Na Boniface Gideon, TANGA
UTEPE wa michauano Kombe la ulinzi Cup umekatwa rasmi jana kwa mchezo mmoja kupigwa katika dimba la Magomeni ambapo timu ya Magomeni Star dhidi Edo Combine kutoka Mwakidila zilikutana na mchezo uliamuliwa kwa mikwaju ya Penati 4-2 baada ya dakika 90 kumalizika milango ya timu zote mbili ikiwa migumu kufunguka
Michauano hiyo iloliyoandaliwa na kudhaminiwa na jeshi la Polisi mkoa wa Tanga itazikitanisha timu 20 kutoka katika mitaa mbalimbali ya jiji la Tanga ikiwa na lengo hasa la kuhamasisha vijana kuachana na matumizi ya madawa ya kulevya.
Akizindua michano hiyo ya mpira wa miguu kwa vijana Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga Henry Mwaibambe alisema michezo kwa sasa ni furaha na ajira lakini lengo lao hasa ni kipenyeza ujumbe kwa jamii kupiga vita matumizi ya madawa ya kulevya.
Aidha alisema sambamba na ujumbe wa michauano hiyo kwa mwaka huu bado jeshi hilo linaendelea kusistiza usalama wa maisha ya watu na mali zao hivyo kuwataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano pale wanapoona Kuna viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani
Michauano hiyo itakayozihusisha timu 20 itachezwa kwa mfumo wa mtoano mpaka bingwa apatikane kwenye fainali huku zawadi mbalimbali zikiwa zinazidi kuvutia timu kuzidi kujipanga zaidi.
Mwisho