Na Shomari Binda-Musoma
VIONGOZI na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha diwani wa Kata ya Mshikamano manispaa ya Musoma, Charles Mwita.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Abubakari Nyamakato amesema wamepokea kwa masikitiko kifo cha diwani Hugo kilichotokea leo asubuhi.
Amesema diwani Mwita ni moja ya madiwani ambao walikuwa wanapendwa na wananchi wake kutokana na kuwa nao karibu.
Nyamakato amesema Chama cha Mapinduzi na wananchi wa Kata ya Mshikamano wamepoteza mtu muhimu na kuwaomba kuwa wavumilivu kwenye kipindi hiki kigumu
Katibu mwenezi huyo amesema chama kwa kushirikiana na familia wataendelea kutoa taarifa juu ya taratibu za msiba huo.
Naibu Meya wa halmashauri ya manispaa ya Musoma Naima Minga amesema wamempoteza diwani huyo mapema wakiwa bado wanahitaji mchango wake.
Amesema hiyo ni mipango ya Mungu na ni safari ya kila mmoja na kumtakia pumziko la milele katika makao mapya.
Diwani Haji Mtete wa Kata ya Nyasho amesema walikuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana kwa katibu na Mwita na kuumizwa na taarifa za kifo chake.
Mmoja wa waendesha pikipiki maarufu bodaboda wanaopaki soko la saa nane Ramadhani Musa amesema hilo ni pigo kwa kuwa Mwita alikuwa mtetezi na msaada kwao.