Home Afya TIGO YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTEKELEZA MKAKATI WA USAJILI WA WATOTO CHINI...

TIGO YAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUTEKELEZA MKAKATI WA USAJILI WA WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO MKOA WA KAGERA

Na Adery Masta

Tangu kuzinduliwa kwa mpango wa usajili wa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ukiwa ni mkakati muhimu ulioanzishwa na Serikali chini ya uratibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa lengo la kuboresha hali ya usajili wa vizazi nchini mwezi Juni, 2015 mpaka sasa watoto zaidi ya 8,292,343  wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.

Akizungumza wakati wa Utambulisho wa Mfumo wa Usajili wa Watoto chini ya Miaka mitano Mkoa wa Kagera , ambao ulihudhuriwa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Pauline Gekul , Joseph Mtalemwa ambaye ni Mkurugenzi wa Tigo Kanda ya Ziwa amesema kuwa 

 “Tigo inayo furaha kwa mara nyingine tena kuendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) na Ubalozi wa Canada nchini Tanzania na wadau wengine wa maendeleo kwa kutekeleza mkakati huo wa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano hapa mkoani Kagera.

Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini Tanzania. Tunajivunia mafanikio ya sekta hii.

Kwa mujibu wa ripoti ya TCRA Q1 2023, kuna zaidi ya watu milioni 61.8 wanaotumia simu za mkononi, zaidi ya milioni 44 wanaotumia huduma za simu za mkononi na zaidi ya watumiaji milioni 33 wa huduma za intaneti. Mafanikio hayo katika sekta ya TEHAMA yamepelekea sekta nyingine kubuni njia rahisi za kufikisha huduma kwa walengwa kwa kutumia teknolojia ya simu za mkononi, na ushiriki wa kampuni ya Tigo katika zoezi hilo muhimu ni mfano hai kuwa usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto umekuwa ukifanyika kwa kurahisishwa na matumizi ya teknolojia ya Simu ya Mkononi.

Sote tunatambua umuhimu wa utambulisho na takwimu katika kuwezesha upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile afya, elimu na kadhalika. Hata katika usajili wa laini za simu tunahitaji kitambulisho halali ambacho chanzo chake ni cheti cha kuzaliwa. Kwa hiyo, umuhimu wa watoto wetu kusajiliwa na kupata vyeti wanapozaliwa ni jambo linalohitaji kupewa kipaumbele cha juu na wadau wote.

Tigo imeendelea kuwekeza katika mradi wa usajili wa watoto tangu 2013 na leo tunatoa simu 600 za ziada. Tunaamini simu hizo zitatumiwa na wasajili waliofunzwa ili kuhakikisha watoto wa mkoa wa Kagera wanasajiliwa, na taarifa zao zinatumwa kwa mfumo wa SMS kwenye mfumo data wa RITA.

Tigo inatambua ukweli kwamba cheti cha kuzaliwa ni kitambulisho cha awali cha mtoto kinachomwezesha kutambua uwepo wake na pia ni haki yake ya msingi. Hivyo basi, tunawahimiza wazazi na walezi kuchangamkia fursa hii na kuhakikisha watoto wote wamesajiliwa na kupewa vyeti.

Kwa mara nyingine tena tunapenda kuwashukuru wadau wote kwa kuendelea kushirikiana nasi, na nichukue fursa hii kuendelea kuihakikishia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wote wa maendeleo kuwa tutaendelea kushiriki katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali na inayolenga hasa katika kuendeleza matumizi ya TEHAMA kwa ustawi wa jamii na uchumi kwa ujumla”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!