Home Afya UCHUNGUZI WA KIIKOLOJIA KUHUSU UGONJWA WA VIRUSI VYA MARBURG WAANZA KAGERA

UCHUNGUZI WA KIIKOLOJIA KUHUSU UGONJWA WA VIRUSI VYA MARBURG WAANZA KAGERA

Na Theophilida Felician, Kagera

Wataalamu kutoka Wizara za kisekta chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wameanza uchunguzi wa Kiikolojia kuhusu ugonjwa wa Virusi vya Marburg baada ya ugonjwa huo kutokomezwa Nchini.

Wataalamu wanaounda timu kutoka ,Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Waziri Mkuu (Menejimenti ya Maafa), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Afya, chuo kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA), Chuo kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori (TAWIRI), na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) wamefika Mkoani Kagera kuanza rasmi kazi hiyo.

Watalam hao ambao wamekutana Mkoani Kagera wanalenga kufanya uchunguzi wa kiikolojia ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya kimataifa ya kufanyika kwa shughuli mbalimbali za ufuatiliaji baada ya ugonjwa huo kudhibitiwa ipasavyo hapa nchini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Prudence Constantine amesema Ofisi ya Waziri Mkuu imeratibu sekta na Taasisi mbalimbali kufanya uchunguzi wa kiikolojia ili kubaini uwepo wa Wanyama wanaoweza kuhifadhi Virusi vya Marburg na mwingiliano wao na wanadamu ambapo Uchunguzi huu ni moja kati ya juhudi za pamoja za kuendelea kujua chanzo cha tatizo, kujiandaa, kukabiliana na dharura za kiafya iwapo zitajitokeza.

“Wizara ya Afya imeainisha uchunguzi huu kati ya kazi muhimu zinazotakiwa kufanyika ndani ya mpango wa siku 90 wa kurejesha hali Mara baada ya mlipuko wa Marburg ulipotangazwa kuisha”.ameeleza Mkurugenzi Prudence

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Mganga Mkuu wa Mkoa huo Dkt. Issessanda Kaniki amesema baada ufuatiliaji wa mbinu za utafiti na vipimo ndani ya siku 42 tumeweza kuudhibiti ugonjwa huo kiiamilifu kama ilivyo kwisha tangazwa hivi karbuni na serikali kupitia waziri wa afya Mhe Ummy Mwaimu.

“Baada ya kufanyika kwa Ufuatiliaji wa hali ya juu kwakutumia mbinu mbalimbali za utafiti Mkoa wa Kagera pamoja na Nchi tunazopakana nazo kwa sasa mlipuko wa Ugonjwa wa Marburg haupo tena”. Amesema Dkt. Kaniki

Uchunguzi huo wa Kiikolojia utakaofanyika kati ya tarehe 12 na 24 Juni, 2023 utahusisha uchukuaji wa sampuli za Wanyamapori, wanyama wa kufugwa pamoja na kufanya utafiti shirikishi jamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Muleba na Kyerwa.

Ikumbukwe kuwa miezi michache iliyopita Mkoa Kagera kupitia kata za Maruku na Kanyangereko Halmashauri ya Bukoba zilikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliopelekea watu sita kupoteza maisha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!