KAMPUNI ya Big Solution watarajia kufanya kongamano maalum la kuwaunganisha pamoja wanaohusika na fani ya kupiga picha mnato na video mapema Juni 6, 2023 katika hoteli ya Mbezi Garden iliyopo Makonde, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Wanahabari leo 26, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Big Solutions, Rajab Mchatta amesema lengo kuu la kongamano hilo ni kuwaleta pamoja na kujadili changamoto zilizopo katika tasnia yao.
Mchatta ameongeza pia kongamano hilo litawakutanisha wapiga picha na wakufunzi ambao watatoa elimu ya masuala ya maadili, fursa za biashara na matumizi ya teknolojia.
Moja wa wapiga picha nguli nchini ambaye ni Mdhamini wa kongamano hilo Mkurugenzi wa DTP Hanif Abdulrasul amesema amevutiwa sana na wazo hilo na kusema kuwa litasaidia wapiga picha kutatua changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo elimu ya kuwekeza katika bima ya vifaa vya uzalishaji picha.
Naye Haika Lawele, Mkurugenzi wa Mbezi Garden Hotel, ambao ni wadhamini wa ukumbi amesema wametoa eneo hilo kuanzia asubuhi hadi jioni ili kufanikisha tukio hilo la kuwakutanisha wapiga picha na kupata elimu ya maadili ya picha ili kuongeza ubora katika kazi zao.
Kongamano hilo limeandaliwa na kampuni ya Big Solutions Limited kwa kushirikiana na kampuni ya Desktop Publishing (DTP), Mbezi Garden Hotel, Jackie Events na Michuzi Media huku wakiomba wito kwa makampuni kujitokeza kuweza kudhamini tukio hilo.
..Mwisho….