Na Mathias Canal, WEST-Iringa
Serikali imesema kuwa haitafanya uzembe kwenye usimamizi wa Ubora wa elimu nchini hivyo imeitaka Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kuhakikisha kuwa inaendeleza udhibiti wa ubora wa elimu nchini katika ngazi ya vyuo vikuu nchini.
TCU imekumbuswa lengo la kuanzishwa kwake ikiwa ni pamoja kuhakikisha inasimamia kwa weledi mkubwa elimu ya vyuo vikuu nchini kwa kufanya utambuzi na uidhinishaji wa elimu ya vyuo vikuu kabla ya chuo kikuu chochote kuanza.
Akizungumza jana tarehe 14 Julai 2022 wakati wa sherehe za siku ya Chuo Kikuu cha Iringa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema kuwa hakutakuwa na shinikizo lolote la utoajia wa Digrii zisizokidhi vigezo kwenye kazi za kitaaluma hivyo serikali itahakikisha kuwa ubora wa elimu unasimamiwa ipasavyo.
Waziri Mkenda amesema kuwa ili kuwe na wataalamu wazuri katika sekta ya afya ni vyema kama kuna uwezekano vigezo viongezwe hususani katika usimamizi wa maswala ya tiba ili kuakisi ubora wa elimu nchini.
“Tukicheza na ubora wa elimu tutaua nchi yetu, na hapa nchini vipo baadhi ya vyuo vya binafsi ambavyo ili viwe na wanafunzi wengi vinatoa GPA kubwa pasina kujali ubora na uwezo wa wahitimu wao” Amekaririwa Prof Mkenda na kuongeza kuwa
“Tanzania sio kapu la kutuletea Digrii feki hivyo ubora wa elimu utasimamiwa bila woga na presha ya watu wenye fedha au wana siasa, lakini na nyie TCU mtoe majibu kwa wakati mkichelewa hatutaelewana”
Prof Mkenda amesema kuwa Vigezo vya udahili na utoaji elimu vinafahamika, ubora unafahamika, hivyo tathmini ikifanyika vikaangaliwa vigezo kila mtu atapata kwa mujibu wa vigezo hivyo na si vinginevyo.
“Nchi yetu haiwezi kuendelea kwa kupeana nafasi kwa undungu, na kwa upendeleo ila tunaweza tukaendelea tukipeana nafasi kwa uwezo, vipaji na juhudi sio kwa sababu baba yako ana hela nyingi ndio upewe hiyo Hapana” Amesisitiza Prof Mkenda
Waziri Mkenda amesema unaweza kuwa na akili nyingi lakini mvivu na mlevi, una uwezo mkubwa lakini mzembe hivyo lazima TCU isimamie ubora na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili elimu ya Tanzania isiwe ni bora elimu bali elimu yenye ubora.