Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amefanya mazungumzo na wataalamu wanaojenga mifumo ya kieletroniki ya Wizara ya Maji, ukiwemo mfumo wa Maji App ambao unawezesha mtumiaji wa simu ya mkononi kupata taarifa mbalimbali zinazohusu Sekta ya Maji kupitia simu janja.
Mazungumzo hayo yamefanyika ofisini kwa Waziri Aweso jijini Dodoma ambapo amewapongeza wataalamu hao kwa uthubutu mkubwa na ubunifu ambao umewezesha kukamilisha mfumo wa Maji App na kuwataka waendeleze ubunifu zaidi katika masuala mtambuka ya Sekta ya Maji.
Amesema maarifa waliyoonesha ni makubwa na yanadhihirisha uwezo mkubwa walionao na kwamba uongozi mzima wa Wizara ya Maji uko pamoja nao na utahakikisha ubunifu zaidi unafanyika ili kuboresha upatikanaji wa taarifa nyingi zinazohusu Sekta ya Maji.
Pamoja na hilo, amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kuwatambua kwa kuwapatia motisha maalumu ili iwe chachu ya juhudi ya kuendeleza maarifa hayo zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Tehama Wizara ya Maji Bw.Joashi Nyitambe ametoa shukran kwa uongozi na kuahidi kufanya muendelezo zaidi wa huduma katika mifumo iliyojengwa. Amesema ushirikiano wanaoupata kutoka kwa viongozi unawatia nguvu na moyo wa kufanya mambo makubwa zaidi.
Timu ya wataalamu hao inahusisha Maafisa Tehama na Watakwinu kutoka Sekta ya Maji ambao walibuni na kujenga mfumo huo ambao ulizinduliwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 Machi, 2022 jijini Da r es Salaam.