Na Magreth Mbinga
Wakala wa Usajili , ufilisi na Udhamini (RITA) wanatarajia kufanya mkutano ambao utakaowashirikisha wadau mbalimbali utakayofanyika Julai 18, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu RITA Angela Anatory amesema kuwa, mgeni rasmi katika Mkutano huo anatarajiwa kuwa Waziri wa katiba na sheria Dams Ndumbaro.
Amesema kuwa, wadau watakaoshiriki katika mkutano huo, watatoka na maadhimio ya nini kifanyike katika utoaji wa huduma zao Ili kuboresha zaidi kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha, amesema miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano ni pamoja kuelezea walipotoka, walipo sasa na wanapokwenda pamoja na mikakati ya kukabiliana na changamoto ambazo wakala wanakutana nazo.
Hata hivyo, Mkutano huo utahudhuriwa na viongozi wa Dini, Wizara mbalimbali, Taasisi za Serikali mabalozi mbalimbali pamoja na wadau wengine ambapo miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na mafanikio walioyapata, Changamoto pamoja na kujiwekea mikakati ambayo itasaidia kuzitatua na kusonga mbele.
Aidha, amesema kuwa, katika eneo la utoaji wa huduma wamebuni program ya Usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano ambapo imefanya vizuri kutoka asilimia 13 hadi kufikia asilimia 65 katika mikoa 23 ya Tanzania Bara ambapo watoto mill 7.7 wameshasajiliwa.
Hata hivyo, ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na Rita ikiwemo kufilisi na kudhamini, kusajili Talaka, ndoa, vyeti vya vizazi na vifo, kusimamia mali ambazo hazina mwenyewe, na za watoto ambao hawajafikisha miaka 18, kusajili mirathi, kuwasili watoto pamoja na kuandika wosia.