Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amewasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati yote ya sekta ya kilimo inayotekelezwa kwenye halmashauli ili kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo na kuongeza tija kwa wakulima.
Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Juni 17, 2022 jijini Dodoma katika Mkutano wa 12 wa wadau wa zao la kahawa na kuwahakikishia wadau wa sekta hiyo kuwa,Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhahakikisha wanasimamia kikamilifu utekelezaji wa mikakati yote ya sekta ya kilimo ikiwemo uzalishaji wa tija na kilimo cha umwagiliaji.
Bashungwa amesema, Ofisi ya Rais-TAMISEMI itaendelea kuimarisha ushirikiano na Wizara ya Kilimo ili kuhakiksha dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo yanatimia kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha vitendea kazi na pikipiki 7,000 kwa Maafisa ugani nchi nzima katika serikali za mitaa vitakavyosukuma maendeleo katika sekta ya kilimo mazao kwa ajili ya ukuaji wa uchumi.
Aidha, Bashungwa amepongeza mfumo wa sasa wa mauzo ya kahawa kufanyika kwa njia ya mnada ngazi ya vyama vya msingi ambao utamkomboa mkulima wa zao hilo na kuondokana na mfumo wa awali uliokuwa unawanufaisha watu wachache na sio wakulima.
Vile vile, amesema tayari amewaelekeza wakuu wa Mkoa wa Kagera, Kigoma, Katavi, Tabora na Pwani kubainisha maeneo ya ardhi ifikapo tarehe 30,Juni 2022 kwa ajili ya kuanzisha uwekezaji wa kilimo cha mazao yatakayosaidia kufikia malengo ya nchi kujitosheleza katika mfuta ya kula.